
Pichani ni baadhi ya dawa bandia zilizokamatwa na kuoneshwa kwa
waandishi wa habari ambao Hawapo pichani Wakati wa kutoka taarifa katika
mkutano na vyombo vya habari Jijini Mwanza Leo

Mkurugenzi mkuu Wa TFDA Hiiti Sillo akionesha Moja ya dawa
bandia zilizokamatwa katika soko Wakati wa mkutano na waandishi wa Habari
Jijini Mwanza.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti usalama, ubora na ufanisi
wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii kwa kuzuia
athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya bidhaa hizi.
Kati ya tarehe 28 Mei na 12 Juni 2012, TFDA ilifanya
Operesheni Maalum katika maeneo mbalimbali Kanda ya Ziwa ikiwa ni
mwendelezo wa Operesheni za kubaini bidhaa duni na bandia kwenye soko kwa
ushirikiano na Jeshi la Polisi nchini pamoja na Ofisi za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Ukaguzi na upekuzi ulifanyika kwenye maduka ya dawa, kituo cha
mabasi ya kwenda mikoani, nyumba za makazi ya watu, nyumba za kulala wageni na
ofisi zinazojishughulisha na kuuza shajala (stationeries).
Lengo la Operesheni hii lilikuwa ni kuwabaini na kuwakamata wale
wote wanaojihusisha na biashara ya dawa duni na bandia kinyume cha Sheria ya
Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 ili hatimaye waweze kuchukuliwa hatua
za kisheria.
*Kufuatia Operesheni hii, dawa mbalimbali bandia zilikamatwa
kama ifuatavyo;
1. Dawa moja yenye majina mawili
tofauti kwenye lebo yaani PRAZIQUANTEL 600mg na AMODIAQUINE HYDROCHLORIDE
200mg. Dawa hii ipo kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 100 na imeghushiwa
mtengenezaji kuwa ni Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) Limited –
Arusha.
Lebo za dawa hii zinaonesha imetengenezwa Oktoba 2011 na inaisha
muda wa matumizi Septemba 2014. Namba ya toleo (batch number) haisomeki vizuri.
Kuna nembo ya MSD pia kwenye lebo za dawa hii. Jumla ya makopo 117 ya dawa hii
yamekamatwa kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo Igoma na duka linalouza
vocha za simu lililoko katikati ya jiji la Mwanza.
2. Dawa yenye jina la kibiashara
SULXINE & PRIMINE na jina halisi SULPHADOXINE & PYRIMETHAMINE (SP).
Dawa hii ipo kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 1000 na imeghushiwa mtengenezaji
kuwa ni Micro Labs Limited – India. Lebo za dawa hii zinaonesha imetengenezwa
Machi 2009 na inaisha muda wa matumizi Aprili 2013. Namba ya toleo (batch
number) ni MRAG024. Namba ya usajili iliyoghushiwa na kuwekwa kwenye lebo ni
TAN 07, 512 JO1E MIC. Makopo mawili ya dawa hii yamekamatwa katika maduka ya
dawa baridi yaliyopo Mkuyuni (Nyamagana) na Nyanguge (Magu) mkoani Mwanza.
3. Dawa yenye jina la kibiashara
DIOSULPH na jina halisi SULPHADOXINE & PYRIMETHAMINE (SP). Dawa hii ipo
kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 1000 na imeghushiwa mtengenezaji kuwa ni Keko
Pharmaceutical Industries (1997) Ltd - Dar Es Salaam. Lebo za dawa hii
zinaonesha imetengenezwa Novemba 2011 na inaisha muda wa matumizi Oktoba 2014.
Namba ya toleo (batch number) ni 051110. Kuna nembo ya MSD pia kwenye lebo za
dawa hii. Makopo mawili ya dawa hii yamekamatwa mikononi mwa mtuhumiwa
aliyekuwa anaisambaza.
4. Aidha, upekuzi uliofanyika
kwenye makazi ya mtuhumiwa mmoja eneo la Sinai (Mabatini) Mwanza umewezesha
kukamatwa kwa lebo kadhaa za dawa bandia aina ya Ephedrin, Dioerythro na
Erythromycin ambapo baadhi yake ziliwahi kukamatwa na TFDA mwaka 2011 na
taarifa kutolewa kwa umma.
5. Vile vile, pamoja na dawa
bandia zilizokamatwa, TFDA ikishirikiana na Jeshi la Polisi na TAMISEMI pia
imekamata dawa moto ambazo haziruhusiwi kuuzwa kwenye maduka ya dawa baridi,
dawa ambazo hazijasajiliwa kutumika nchini, dawa za Serikali na dawa
zinazotumika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma ambazo haziruhusiwi kuuzwa
kwenye maduka ya dawa binafsi.
0 comments:
Post a Comment