idraji Ibrahim na Israel Mugusi, Dodoma
HATMA
ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba inatarajiwa
kujulikana kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho
kinachoanza leo.
Kikao hicho kinaanza asubuhi hii mjini hapa, huku kukiwa na taarifa kuwa sekretarieti yake huenda ikavunjwa.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ya CCM, zinadai kuwa uamuzi
huo unachukuliwa ikiwa ni hatua ya chama hicho kujivua gamba
linaloonekana kuchuja mbele ya umma.
Chanzo
chetu cha habari kilidai kuwa, baada ya kuvunjwa sekretarieti, Makamba
ambaye ndiye mwenyekiti wa sekretarieti hiyo, atawasilisha taarifa ya
kuomba kustaafu.Hatua hiyo inamwezesha Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete kuteua sekretarieti nyingine ambayo itakiongoza hadi mkutano
mkuu unatarajiwa kufanyika mwakani.
Makamba amekuwa akituhumiwa kusababisha chama hicho kufanya vibaya kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
Anatuhumiwa kutoa kadi kwa baadhi ya wagombea wa chama hicho ambazo
zilitumika kuingiza wanachama mamluki na kuruhusu kila mwanachama wa CCM
kupiga kura ya maoni.
Halmashauri
kuu ilikuwa imeagiza kura za maoni ndani ya chama hicho zihuhusishe
wanachama hai, lakini aliagiza kila mwanachama kushiriki bila kujali
kama ni hai au hajalipia kadi yake.
Kulingana
na kanuni za chama hicho, iwapo sekretarieti hiyo itavunjwa, licha ya
Makamba watakaopoteza nafasi zao ni Naibu Makatibu wakuu CCM bara na
Zanzibar, George Mkuchika na Saleh Ramadhan Ferouz, Katibu wa Itikadi na
Uenezi, John Chiligati; Katibu wa Mipango, Kidawa Saleh na Katibu wa
Kitengo cha Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wanaotajwa
kuchukua nafasi ya Makamba ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Habari, Ajira,
Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi huku ikidaiwa kuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM, Abdulrahman Kinana amekataa nafasi hiyo. Mwingine
anayetajwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wassira lakini inadaiwa kuwa kasoro inayomkumba ni pale
alipokihama chama hicho na kwenda NCCR-Mageuzi.
Akipokea
wanachama wapya kutoka Chadema jana, Rais Kikwete alisema kikao hicho
ni muhimu kwa chama chao huku akiwaomba radhi wanachama kwa matokeo ya
Uchaguzi Mkuu na kuwataka wasahau yaliyopita, wagange yajayo.
“Tunaanza
vikao muhimu vya kujenga chama chetu,” alisema Rais Kikwete.Wanachama
wapya waliojiunga na CCM ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Mbeya, Shambwele Shitambala na Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya Ileje,
Henry Sayuni.Rais Kikwete alisema Tanzania ina vyama vingi, lakini
ukweli utabaki kuwa CCM ndicho makini huku akisema vingine siyo vyama,
bali mkusanyiko wa wanaharakati.
CHANZO:MWANANCHI
|
0 comments:
Post a Comment