Waandishi Wetu
WAKATI
dawa aliyoigundua Mchungaji Ambilikile Mwasapile ikionekana kuwavuta
watu karibu nchi nzima kutaka kuinywa, baadhi ya wakazi wa Arusha
wameamua kwenda maporini kusaka dawa hiyo.
Taarifa
ambazo pia zimemfikia mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), zimeeleza kuwa watu hao tayari wamevamia pori
la mlima Sonjo kuchimba dawa anayotumia kutibu.Hata hivyo, Mchungaji
Mwasapile alisema haitawasaidia kwa vyovyote kwa sababu ni yeye pekee
aliyepewa uwezo na Mungu ili awaponye watu.
Hata hivyo, Mchungaji Mwasapile, ameiomba Serikali kuingilia kati kwa
kuwadhibiti watu hao, aliowaita kuwa ni matapeli ambao tayari wamevamia
pori hilo kwa sababu watasababishawatasababisha watu wengine kuikosa kwa
vile uchimbaji utakuwa ni wa vurugu na pia utasababisha uharibifu wa
mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari, mchungaji huyo alisema watu hao,
wamekuwa wakiwatumia baadhi ya vijana wa kijiji cha Samunge ambao
wanaujua mti wa Mugariga, au Mungamuryogo na wameanza kuchimba mizizi na
kusafirisha nje ya kijiji hicho.
"Naomba nitoe angalizo, hii dawa ni mimi pekee ndiye Mungu ameniotesha
kuitoa na inakwenda pamoja na maombi sasa hawa wanachimba mizizi na
kwenda kutengeneza haitawasaidia ni utapeli," alisema Mchungaji
Mwasapile.
Mchungaji huyo aliiendelea kuiomba Serikali kukarabati miundombinu ya
kufika katika kijiji cha Samunge kwa sababu sasa mvua zimeanza kunyesha
na kwamba siku si nyingi barabara za kumfikia zitakuwa hazipitiki.
Kutokana na ubovu wa barabara hiyo, gari lililokuwa limembeba Waziri
Mkuu Mstaafu lilikwama juzi jirani tu na kwa mchungaji huyo sambamba na
magari mengine kadhaa.
Kukwama kwa magari hayo, kulitokana na mvua ambazo zimeanza kunyesha na
kuharibu barabara ya kwenda katika kijiji hicho, inayotokea eneo la
Kigongoni Mto wa Mbu, kupitia kata za Selela, Engaruka na Ngaresero.
Magari mengi yalikuwa yameharibika na kukwama kati kati ya miti juzi,
hali ambayo inatishia usalama wa barabara hiyo ambayo ni ya vumbi.
Akizungumzia barabara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa
Lali, aliwataka madereva kuwa makini ili kuzuia mfululizo wa ajali.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapile alirudia tena onyo lake la
kuwataka watu kuacha kuwapeleka kwake wagonjwa waliotoroshwa hospitali
huku wengine wakiwa na chupa za kuongezewa maji mwilini.
"Wanakuja huku wakiwa na Dripu za maji. Sasa hapa sio hospitali ya
rufani. Wagonjwa waletwe hapa kwa tahadhari kubwa kwanza barabara zetu
sio nzuri," alisema Mwasapile.
Idadi ya magari na watu toka ndani na nje ya nchi inaongezeka katika
kijiji hicho na sasa kupata dawa mgonjwa inachukuwa kati ya siku mbili
hadi tatu.
Mwandishi wa habari hizi juzi alishuhudia wagonjwa toka nchi za Kenya,
Zambia, Malawi, Uganda na Afrika Kusini wakiwa wamepanga foleni ya
kupata dawa.
Madaktari wa Moshi
Kutoka Moshi, madaktari mbalimbali wameitaka Serikali kuandaa kongamano
la wanasayansi kujadili tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapile, ikiwamo
kutolewa kwa ripoti za kisayansi za wagonjwa waliopona. Wakizungumza na
Mwananchi, madaktari hao wamedai kisayansi haiwezekani kupima dawa
inayotokana na imani ya dini, lakini ni vyema wakapatikana wagonjwa
wanaodai kupona wakiwa na kumbukumbu za matibabu ya siku za nyuma.
Mmoja wa madaktari bingwa, Profesa Waitoki Nkya, ambaye sasa amestaafu
serikalini alisema Taifa bado liko gizani kuhusu ukweli wa nguvu ya dawa
hiyo katika kutibu magonjwa sugu ukiwamo Ukimwi, kisukari na saratani.
“Binafsi siamini katika jambo hilo lakini, naishangaa Serikali na
vyombo vyake kwamba kweli vimeshindwa kutuambia mgonjwa X wa Ukimwi
alikuwa na CD4 200, baada ya kunywa zimeongezeka hadi 1,000?” alijoji.
Profesa Nkya ambaye aliwahi kufanya kazi Hospitali ya Rufaa ya KCMC na
kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kabla ya kustaafu, alisema taifa
linaweza kuondokana na giza hilo kwa wataalamu kuthibitisha nguvu ya
dawa hiyo.
Profesa Nkya alisema Tanzania kama Taifa haliwezi kuruhusu watu
waliokunywa dawa hiyo kujisemea wenyewe kuwa wamepona wakati hakuna hata
mmoja anayethubutu kutoa vipimo vya awali na vya sasa kuthibitisha
amepona.
Hata hivyo, daktari mmoja ambaye ni mratibu wa Ukimwi kwa zaidi ya
miaka 10 sasa, alisema katika suala la Ukimwi bado hajathibitisha nguvu
ya dawa hiyo isipokuwa kwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu
(BP).
“Kwa kisukari na BP naweza kusema kuna mafanikio kidogo kwa sababu kuna
wagonjwa wetu wa kisukari walikuwa katika hatua ya kudungwa sindano
kila siku lakini, sasa wana wiki hawajachoma sindano na wako vizuri,”
alidai.
Daktari mwandamizi katika Hospitali ya Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi, Dk
Issa Mbaga, ambaye alisema anatoa maoni binafsi na sio ya Taasisi yake,
alisema tatizo ni waliokunywa dawa kutopima upya kuthibitisha kupona.
“Unajua ni vigumu kupima jambo kiimani kama ilivyo kunywa dawa ya Babu
kule Loliondo lakini, hawa waliorudi na kutuambia wanaendelea vizuri kwa
nini wasipime upya wakatupa ripoti?” alihoji Dk. Issa.
Wazidi kwenda Loliondo
Wakati huo huo, kitimutimu cha wananchi kutaka kwenda huko kimesikika
karibu kila mkoa hapa nchini ila tatizo kubwa ni gharama za usafiri
pamoja na chakula.Katika Manispaa ya Shinyanga watu wengi wamejitokeza
kwenda kujiandikisha ili waende Loliondo baada ya kupata taarifa kuwa
Mbunge wao, Steven Masele amekusudia kuwagharimia usafiri.
Wananchi hao walikusanyika jana kwenye ofsi ya mbunge kujiandikisha na
awamu ya kwanza ya kundi la watu hao ilitarajia kuondoaka
jana.Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu mbunge huyo alisema kuwa
amegharimia safari hiyo bila kujali wanaoenda ni wagonjwa au la.
Hata hivyo, alisema wale wenye uwezo washiriki watapaswa kuchangia kiasi
kidogo cha fedha ili kutoa nafasi ya watu wengi wanaomiminika katika
ofisi yake ili kujiandikisha kwa safari.
Mwanza nako
Jijini Mwanza nako watu wengi wamesikika wakitaka kupata tiba hiyo
miongoni mwao ni wafanyakazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambao
tayari wameanza kuchangishana ili kugharimia safari.
Habari zilizopatikana toka ofisi ya mkuu wa mkoa huo na kuthibitishwa na
Ofisa Usafirishaji wa Mkoa, William James zilieleza kwamba wafanyakazi
hao wamekusudia kwenda kabla ya kufika mwishoni mwa mwezi huu.
James alisema hadi jana wafanyakazi 26 walikuwa wamejiorodhesha kwenda
na kila mmoja tayari amelipa Sh80,000.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbasi
Kandoro, alielezea kuwa hahusiki katika mpango huo kwa sababu hiyo ni
safari binafsi.“Hii siyo suala la ofisi ni wafanyakazi binafsi, ndiyo
maana uliponiuliza nilishangaa na kwa vile mimi sikuwepo nilikuwa sijui
lolote," alisema Kandoro.
Morogoro nao wamo
Kutoka mkoani Morogoro, inaripotiwa kuwa Watu Wanaoishi na Virusi vya
Ukimwi (Wavumo) wamemwomba mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, Aziz
Abood kuwapa msaada wa kuweza kufika Loliondo ili kupata dawa ya
'Babu'.Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Wavumo,
katibu wa kikundihicho, Said Shija alisema kuwa wao nao wamehamasika na
dawa hiyo.
Alisema kuwa wao wana imani na dawa hiyo na kwamba kinachowashinda hadi
sasa kufika huko Loliondo ni kwamba hawana uwezo na kumudu gharama za
usafiri.
Askofu Kakobe
Jijini Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Full Gospel Fellowship,
Zacharia Kakobe, ameendelea kutoa maneno ya shutuma dhidi ya mchungaji
Mwasapile.
Hii ni baada ya Mwasapile kusema kwamba anawakaribisha ili kunywa dawa
hiyo licha ya kumdharau pamoja na tiba anayoitoa. Kakobe amerusha
kombora lingine akidai haendi ng’o na yeye sio nyasi zinazotikiswa na
upepo kama watu wengine wanaokwenda huko.
Mwasapile maarufu kwa jina la ‘Babu’ aliwajibu viongozi hao waliomtuhumu
kuwa tiba anayoitoa ni ya nguvu za giza, akisema kuwa waliotoa tuhuma
hizo wana mtazamo wa kifedha zaidi na sio imani.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Askofu Kakobe alisema kwanza
anawahurumia wanaoendelea kwenda huko kwa sababu tayari wameshatekwa na
huduma hiyo ya 'kitapeli.'
“Siwezi kwenda kunywa dawa hata kidogo, kwa sababu mimi sio nyasi
zinazotikiswa na upepo kama wengine waliokwenda huko,” alisema Askofu
Kakobe.
Ajali Loliondo
Kwa upande mwingine, ajali za magari yanayoenda, au kutoka kwa 'Babu' nazo zinaendelea kuongezeka.
Jumatano iliyopita mtu mmoja alikufa na wengine watano kujeruhiwa baada
ya gari lililokuwa njiani kwenda Loliondo kupasuka tairi na kupinduka
eneo la Makuyuni, wilayani Monduli.
Ajali hiyo inafanya idadi ya watu waliokufa tokea msururu wa watu toka
pembe zote za nchi walipoanza kumimika katika kijiji cha Samunge,
Wilayani Ngorongoro kufiki saba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo. Alisema ajali hiyo ilitokea saa nane mchana
kufuatia kupasuka kwa gurudumu la nyuma la gari hilo, kisha kupinduka.
Alimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Fatuma Badru (34), mkazi wa Soweto mjini Moshi.
Aliwataja majeruhi kuwa ni Ruth Lyimo, Mary Sembugao na Salma Badru na mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Omary.
Habari hii imeandikwa na Mussa Juma-Loliondo, Daniel Mjema-Moshi, Suzy
Butondo-Shinyanga, Frederick Katulanda-Mwanza, Filbert Rweyemamu-Arusha,
Lilian Lucas-Morogoro na Elizabeth Suleyman - Dar.
|
0 comments:
Post a Comment