MTU mmoja ambaye ni mkuu wa shule ya sekondari ya Ismila katika wilaya ya Iringa vijijini Pangras Msasamela amekufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa vibaya huku abiria zaidi ya 40 wakinusurika kifo baada ya basi la Hekima lenye namba za usajili T 399AVU linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam -Mbeya kugongana uso kwa uso na gari ndogo yenye namba T 746 AKU Toyota Mark II leo
Ajali hiyo ilitokea jioni hii katika eneo la Kibwabwa Manispaa ya Iringa wakati basi hilo la Hekima likiwa safarini kuelekea mkoani Mbeya.
Abiria wa basi hilo la Hekima ambao walionusurika kufa katika ajali walimweleza mwandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hiyo ndogo ambaye alihama upande wake na kutaka kukatisha upande wa kulia bila kutazama basi hilo mbele .
Alisema Kevin Mwakasumile kuwa dereva wa basi hilo alifanya jitihada mbali mbali za kutaka kulikwepa gari hilo ila bado dereva wa gari ndogo aliendelea kuyumba barabarani hadi magari hayo yanapogongana uso kwa uso.
" Kweli dereva wa basi amefanya jitihada kubwa sana za kuokoa maisha ya sisi abiria tuliokuwemo ndani ya basi hili ...kwani kama dereva angelikuwa mzembe katika basi hili letu hakuna mtu ambaye angepata kutoka mzima ....ujue basi lilikuwa likielekea kupinduka kabisa"
Hata hivyo alisema katika ajali hiyo abiria wa basi walinusurika kifo huko baadhi yao wakipata michubuko midogo midogo mwili kutokana na kukanyagana ndani ya basi hilo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa mtu mmoja ndiye aliyepoteza maisha katika ajali hiyo .
0 comments:
Post a Comment