Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewatoa hofu wananchi wake kuwa limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote nchini Tanzania wanashehereka sikuku ya Krismasi na Mwaka mpya kwa amani na utulivu katika swala zima la ulinzi hasa maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Akizungumza kwa niaba ya kamishna mkuu wa polisi, Kamishna wa Oparesheni na mafunzo Bw. Paulo Chagonja amesema katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Pia amesema kutokana na hali iliyojitokeza mwaka jana mkoani Tabora kwa watoto wenye umri mdogo kuingia kwenye kumbi za disco maarufu kama disco toto kupatwa na tatizo la vifo amepiga marufuku kwa wamiliki wa kumbi mbalimbali za starehe kuingiza watoto wadogo ambao wako chini ya umri unaotakiwa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na swala zima la baadhi ya wamiliki wa kumbi za starehe kuwatumia watoto wa kike kama biashara amesema kuwa ni kosa kubwa tena haramu na kwa yeyote atakayepatikana akifanya vitu kama hivyo aripotiwe haraka ili jeshi la polisi lichukue mkondo wake. Akihitimisha katika maswali DCI Bw. Robert Manumba amegusia swala la Mh.Zitto Kabwe kutishiwa kuuawa ambapo amesema kama Mh.Zitto alitishiwa kuuawa ofisi za serikali zinazoshughulikia maswala haya ziko wazi na watu wote waliona taarifa na ushahidi wa kutosha waripoti.
0 comments:
Post a Comment