Watatu wafariki 19 wajeruhiwa katika ajali
Watu watatu wamefariki dunia papo hapo na wengine 19 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka katika eneo la Ukiriguru wilayani Misungwi mkoani Mwanza.Kamanda wa Polisi mkoa Mwanza, Jamal Rwambow, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 1.58 asubuhi ambapo ililihusisha basi la kampuni ya Bedui lenye namba za usajiri T 473 AJY.
Kamanda Rwambow alisema basi hilo lillikuwa likisafiri kutoka Shirima wilayani Misungwi kuelekea jijini Mwanza ambapo kutokana na mwendo kasi lilimshinda dereva na kuacha njia kisha kupinduka.
Aliwataja walikufa papo hapo kuwa ni pamoja na dereva wa basi hilo aliyejulikana kwa jina moja la Mohamed mwenye umri wa kati ya miaka 30 na 33, Utingo aliyejulikana kwa jina la Francis james (37) na mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja anayekadiriwa kuw na umri wa kati ya miaka 20 na 25.
Alisema majeruhi nane ambao hali zao zilikuwa mbaya wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando wakati wengine walitibiwa katika hospitali ya wilaya ya Misungwi na baadhi kuruhusiwa.
Waliokimbizwa Bugando ni pamoja na Samwel William ( 44), Susan Gasper (30) na Godfrey Samwel (2) wakazi wa Hungumarwa.
Wengine ni pamoja na Shiogo Daudi (32), Nyemela Dogasi (21), wakazi wa shirima, Alex Bwire (30) na Enock Ruta (24) ambao ni wakazi wa Mahopa pamoja na Ixbrahimu Mohamed (32) mkazi wa Igoma jijini Mwanza ambao wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Kamanda Rwambow amewataka wananchi na abiria washirikiane na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa ama kupiga simu pale wanapoona dereva anaendesha kwa mwendo kasi ili gari liweze kukamatwa kabla ya madhara makubwa kutokea.
0 comments:
Post a Comment