Mshindi wa Bongo Star Search (BSS) kwa mwaka 2009, Pascal Cassian almaarufu kama Baba Rita, ametoa mpya baada ya kujikuta akiwashukuru Watanzania kwa zaidi ya mara 12!
Cassian, alilazimika kupagawa kwa furaha baada ya kutangazwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho kilichowashirikisha wakali lukuki, huku yeye akizoa maelfu ya kura za Watanzania na kuwaacha mbali wenzie.
Washiriki watano ndio walioingia kwenye fainali za kinyng'anyiro hicho, ambazo zilifanyika usiku wa kuamkia leo katika ukumbi ulioshonana watu wa Diamond Jubilee, pale Upanga Jijini.
Baada ya kutangazwa mshindi na Jaji Mkuu Ritha Paulsen (Madam Rita), na hivyo kujihakikishia zawadi ya kwanza ya fedha taslim kiasi cha shilingi milioni 25, Cassian alijikuta akigubikwa na furaha ya aina yake na hivyo kuwashukuru zaidi ya mara kumi na mbili Watanzania ambao kupitia kura zao, ilidhihirisha wazi kuwa yeye ndiye kipenzi na chaguo lao la kwanza.
“Nawashukuru Watanzania, Nawashukuru Watanzania, nawashukuru Watanzania…naomba tuimbe kwa pamoja... Shebeneza,” akasema huku akibubujikwa na machozi ya furaha.
Baada ya kumaliza kuimba wimbo huo, Cassian ambaye kwa mujibu wa kura zilizokuwa zikitangazwa katika ukumbi huo alionekana kuwazidi mno wapinzani wake, aliendelea kuwashukuru Watanzania tena na tena, huku akieleza ukweli kuwa bila wao, kamwe asingefikia alipo .
Katika fainali hizo za usiku wa kuamkia leo, mshindi wa pili alitangazwa kuwa Peter Msechu, ambaye ni mshiriki toka Kigoma. Yeye alijinyakulia kitita cha shilingi milioni tano.
Aliyefuatia ni Kelvin Mbata kutoka Jijini Dar es Salaam, ambaye alipata shilingi milioni tatu, huku wa nne na wa tano wakiwa ni Jackson George toka Tanga na Beatrice William wa Mwanza.
Awali, dalili za kukubalika zaidi kwa Cassian ambaye ni mshiriki toka Mwanza zilianza kuonekana mapema, pale Jaji mkuu Rita alipokuwa akilazimika kusimama kila alipopanda msanii huyo, ikiwa ni kutekeleza rai za mashabiki ambao walikuwa wakimshinikiza kufanya hivyo, kama ishara ya kumkubali zaidi.
Pata picha na taarifa zaidi za BSS katika kurasa za kati na pia ukurasa wa 16 wa gazeti hili.
0 comments:
Post a Comment