Majambazi yazidiwa ujanja
Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamempiga risasi na kumjeruhi vibaya mfanyabiashara mmoja wa madini na kisha kumpora gari na fedha.
Hata hivyo wananchi kwa kushirikiana na Polisi walifanikiwa kuliokoa gari hilo na kuyang'anya majambazi hayo shehena ya silaha za kivita.
Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Elias Kalinga amesema tukio hilo la aina yake limetokea juzi mishale ya saa 2:00 usiku katika kijiji cha Mwanangwa wilayani Misungwi.
Akamtaja mfanyabiashara aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni na kisha kuporwa gari na fedha kuwa ni Majid Amir, maarufu kwa jina la Ahamed, mkazi wa mjini Shinyanga.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kalinga amesema dalili zinaonyesha kuwa watu hao walianza kumfuatilia Bw. Ahamed ambaye alikuwa akienda kwenye machimbo ya almasi katika kijiji cha Mwanangwa wilayani Misungwi.
Akasema Mfanyabiashara huyo alipofika kijijini hapo alivamiwa na watu hao ambao walimpiga risasi katika mguu wake na kumpora gari na fedha kisha wakakimbia kwa uelekeo wa Mwanza.
Kamanda Kalinga akasema baada ya taarifa kumfikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Misungwi, alianza kupiga simu na kutuma meseji kwa vituo vingine vya polisi ili waweke vizuizi barabarani.
Akasema taarifa hizo zilisambaa kwa haraka ambapo ziliwafikia wananchi wa kijiji cha Kulumindia, ambao walifunga barabara kwa kupanga magogo.
Akasema gari hilo lilipofika kwenye kizuizi hicho cha magogo lilisimama na ndipo wananchi walipochomoa ndani ya gari na kuanza kuwashambulia watu hao kwa kuwapiga na mawe na silaha nyingine za jadi.
Akasema hata hivyo mmoja wa majambazi hao alitumia bastola kufyatua risasi hewani na wananchi wakatawanyika na kuwapa upenyo wa kukimbilia kusikojulikana huku wakiliacha mahalihapo gari walilopora.
Akasema wananchi hao kwa kushirikiana na Polisi waliokuwa katika eneo hilo, walifanikiwa kuokoa gari hilo na kuwanyang'anya silaha walizokuwa nazo.
Kamanda Kalinga akazitaja silaha hizo kuwa ni bunduki moja aina ya Short Machine Gun, iliyokuwa na magazine tatu.
0 comments:
Post a Comment