.jpg)
Serikali imeionya kampuni ya Rites kutoka India inayokodisha injini na mabehewa kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuacha kutoa vitisho kwamba itavunja mkataba na kuchukua vifaa vyake.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana baada ya kikao cha juzi kati ya Rites, TRL, Serikali na uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), onyo hilo lilitolewa baada ya kampuni hiyo kutoa vitisho kwamba itavunja mkataba wa kukodisha mabehewa yake kwa TRL, kama haitalipwa dola za Marekani milioni 12.36 inazodai.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu, Injinia Omar Chambo, alisema ofisi yake imepokea barua kutoka Rites inayotoa vitisho hivyo kwamba itavunja mkataba huo iwapo haitalipwa hadi kesho.
Hata hivyo, Chambo hakutaka kueleza kwa undani hatua ambazo serikali itachukua kama itashindwa kutekeleza sharti hilo, lakini alisema serikali inajua itachukua hatua gani.
“Tumepokea barua rasmi kutoka Rites lakini hatua gani tutachukua hiyo sio kazi yako bali hiyo ni kazi yetu serikali,” alisema.
Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Trawu, Silvester Rwegasira alisema, wameamua kusitisha mgomo wao baada ya kukutana na serikali na kufanya nao mazungumzo.
Alisema moja ya madai ya wafanyakazi wa lililokuwa Shirika la Reli Nchini (TRC) kabla ya kubinafsishwa ya kutaka kusainiwa mkataba wa hiari ambapo mfanyakazi atatakiwa kulipwa fedha kama mkono wa heri.
Wafanyakazi hao walitaka mkataba huo usainiwe kabla ya kuingia katika ajira mpya na TRL ambayo ina ubia na serikali.
Kampuni ya TRL ni ubia ambapo serikali ina hisa za asilimia 49 na mwekezaji kutoka nchini India asilimia 51.
Mkurugenzi Mtendaji wa Rites, Vinay Kumar Agarwal juzi alikaririwa akisema kuwa kampuni yake iliingia mktaba wa kuikodishia TRL injini 25 na mabehewa 23 Julai mwaka juzi.
Katika mkataba huo Rites ilidai serikali ilikubali kulipa malipo hayo kidogo kidogo kila baada ya miezi mitatu.
0 comments:
Post a Comment