
Wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari (Kibasila), leo asubuhi wamefunga kwa muda barabara za Mandela na Chang'ombe kwa staili ya kulala barabarani, lengo likiwa kushinikiza eneo hilo kuwekewa matuta au taa.
Tukio hilo limefanyika kuanzia mishale ya saa 3:30 asubuhi na kusababisha foleni kubwa ya magari katika barabara hizo.
Mwandishi wa gazeti hili ameshuhudia wanafunzi hao wakiwa wamepanga mawe, majani na wao wenyewe kulala katika makutano ya barabara hizo, eneo ambalo ni maarufu kwa jina la Machinjioni, kutokana na ajali za mara kwa mara zinazotokea katika eneo hilo.
Hali hiyo ilisababisha magari kushindwa kupita, hali iliyoleta usumbufu mkubwa kwa watu waliokuwa wakiwahi makazini.
Baada ya wanafunzi hao kufunga barabara hizo kwa muda, gari la Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia, FFU, lilifika eneo hilo, lakini wanafunzi hao wakaanza kulizomea huku wakipiga kelele za kutaka wasikilizwe.
Baadhi ya wanafunzi hao wamedai kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa matukio ya wezao kugongwa mara kwa mara katika eneo hilo.
"Wenzetu kibao wamegongwa katika eneo hilo, wengine wamekufa na wengine wamekuwa vilema, tumelalamika sana lakini hawatusikii ndio sababu leo tumeamua kufunga barabara," akasema mwanafunzi mmoja kwa sharti la kutotaja jina lake.
Alasiri ilipomtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke ili kuzungumzia tukio hilo, hakupatikana mara moja kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila majibu.
Aidha Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alhaj Suleiman Kova naye simu yake ilikuwa ikiita bila kujibiwa.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, wanafunzi hao walikuwa bado wakiendelea kufunga barabara hizo na hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyekuwa amefika katika eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment