TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Friday, September 11, 2009

Lipumba adai Rais Kikwete hawezi kukwepa kashfa za ufisadi

12:46 PM

MWENYEKITI wa CUF, Ibrahim Lipumba amesisitiza msimamo wake kuwa Rais Jakaya Kikwete hawezi kukwepa tuhuma za ufisadi zinazowakabili watendaji wa serikali yake, baada ya mkuu huyo wa nchi kusifu rekodi yake ya vita dhidi ya rushwa katika mazungumzo yake na wananchi juzi.

Lipumba alikuwa ni mmoja wa watu waliofuatwa na Mwananchi kutoa maoni yao kuhusu mazungumzo hayo ya Rais Kikwete aliyoyafanya kwa njia ya televisheni, akijibu maswali yaliyoulizwa moja kwa moja na wananchi kwa njia ya simu, barua pepe na ujumbe mfupi wa simu (sms), ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya nne kutumia njia hiyo ya aina yake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alisifu hatua ambazo serikali yake imechukua kupambana na ufisadi, akitaja kesi 25 zilizo mahakamani kuwa ni kielelezo tosha cha historia ambayo imewekwa katika vita dhidi ya rushwa.

Lakini Prof Lipumba alisema licha ya kupambana na ufisadi, Rais Kikwete hawezi kukwepa kashfa ya utoaji zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development, ambayo ilisababisha Edward Lowassa kuachia uwaziri mkuu mapema mwaka jana.

Akichambua mazungumzo hayo, Lipumba alisema Kikwete hawezi kujinasua na mzimu wa ufisadi unaoendelea kuitesa nchi, ikiwa ni pamoja na kashfa ya Richmond na wizi kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

“Baraza la mawaziri linashauri na rais anafanya maamuzi, kwa hiyo maamuzi yaliyofanywa na baraza kuhusu mkataba wa Richmond, yasingeweza kutenguliwa na mtu mwingine yeyote zaidi yake,” alisema Prof Lipumba, ambaye ni mchumi.

“Rais Kikwete hana maelezo ya kuwaridhisha wananchi kuhusu kashfa ya Richmond..., kwa sababu tumepata hasara kubwa kama taifa, tumekosa mapato na kupoteza mapato kwa maamuzi ya kizembe. Rais hawezi kujinasua katika mzimu wa ufisadi nchini.”

Alifafanua kwamba aliitahadharisha serikali kuhusu kuifanyia uchunguzi Richmond kujua uwezo wake kabla ya kuingia mkataba, lakini hawakumsikiliza.

Lipumba alisema Richmond ilishapewa zabuni ya mradi wa kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es salaam hadi Mwanza mwaka 2004, lakini ikashindwa, "inakuaje tena inarudi na kupewa mradi mwingine mkubwa zaidi na wizara ileile chini ya waziri yuleyule".

Prof Lipumba alisema kuna maofisa ambao wanajulikana kuwa waliisababishia serikali hasara katika kupitisha mkataba wa Richmond, lakini kutokana na urafiki na kujuana, hawajafikishwa mahakamani.

Alihoji sababu za mwanasheria wa zamani, Andrew Chenge kutochukuliwa hatua licha ya kutajwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema hakuna urafiki wala undugu katika vita hiyo na kwamba baadhi ya watuhumiwa hawajafikishwa mahakamani hadi sasa kutokana na uchunguzi dhidi yao kuwa mgumu na kuahidi kuwa kesi tatu kubwa zinaweza kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Kuhusu suala la muafaka baina ya CCM na CUF, Profesa Lipumba alisema Rais Kikwete ameshindwa kutoa majibu sahihi ya suala hilo na kuhoji sababu za mambo makubwa kama marekibisho ya katiba na tume ya uchaguzi kupelekwa kwa wananchi.

Nayo Chadema imebeza mtindo huo mpya wa Kikwete wa kufanya mazungumzo na wananchi kwa njia ya simu na kuuelezea kuwa ni kupima kasi ya maji kwa mguu.

Naibu katibu mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Hamadi Yusuf alisema kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa kisiasa kuwa anajipigia kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani.

“JK anaendeleza ujanja wake... anataka kupima maji kwa mguu. Ni kweli wananchi watapata nafasi ya kutoa madukuduku yao, lakini kwa sasa hataweza kutekeleza chochote kwa mwaka mmoja uliobaki kama ameshindwa kwa miaka minne aliyokaa madarakani,” alisema Yusuf.

Hata hivyo, wasomi walikuwa na maoni tofauti wakisema majibu mengi yalikuwa ya kisiasa huku wengine wakidai kuwa watu waliopata nafasi ya kuuliza maswali, waliandaliwa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mwesiga Baregu alisema maswali aliyoulizwa Kikwete yalipangwa na kusisitiza kuwa waraka uliondaliwa na viongozi wa dini nchini kwa ajili ya kuwaelimisha waumini wao kuchagua viongozi bora, hauwezi kuibua suala la udini nchini kama ilivyodaiwa na mkuu huyo wa nchi.

“Hapa lazima ieleweke kuwa nia ya Waraka ni kuweka wazi maadili ya viongozi wanaotakiwa kuchaguliwa, sasa hapa mgawanyiko utaletwa na lipi,” alihoji Baregu.

Akizungumzia majibu ya Rais Kikwete kuhusu kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Dar es Salaam(RCO), Abdallah Zombe kuachiwa huru, Baregu alisema “majibu hayakuridhisha, yalijaa siasa nyingi na kwamba jaji alisema wazi kuwa wauaji hawakupatikana sasa mbona hilo hakulizungumza”.

Alisema: “Kuhusu suala la safari za nje pia ilikuwa ni siasa tupu, rais ilitakiwa atueleze wazi kwa sababu sio anazungumzia mikataba tu, lakini hatuelezi wazi hao wanaotoa mikataba wanapata nini kwa sababu inawezekana maslahi yao yakawa makubwa kuliko ya Watanzania.

Hata suala la ufisadi halikuwekwa wazi ilitakiwa Rais atueleze waliochukuliwa hatua, sio wingi wa kesi mahakamani.”

Naye Dk Senkondo Mvungi alisema ingawa Kikwete amekumbuka kuongea na wananchi wakati muda umekwisha, hata maswali aliyoulizwa aliyajibu kisiasa.

“Kuhusu suala la Zombe, nilitegemea kuwa Kikwete atajibu kuwa polisi walimzunguka, lakini kwa jinsi alivyojibu nilishangaa sana,” alisema Mvungi.

Wananachi wa kada nyingine, walisema hakukuwa na mfumo mzuri wa kupiga simu na hivyo watu wengi hawakupata fursa ya kuweza kuuliza maswali yao.

Mjini Dodoma, ofisa habari wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Angela Msimbila alisema rais amefanya jambo jema kwa kuwa ujumbe wa wananchi umemfikia moja kwa moja bila kupitia kwa mtu mwingine.

Wakati huohuo, Rais Kikwete amewashukuru wananchi wote na vyombo vya habari kwa kufanikisha mazungumzo kati yake na Watanzania.

“Nimefurahi na nimefarijika sana kwa kupata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi kwa namna ya kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao, kupata hoja zao na maoni yao kuhusu mustakabali wa nchi yetu, serikali yetu, na maendeleo yetu,” inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.

Imeandikwa na Salim Said, Fredy Azzah, Joyce Mmasi, Fidelis Butahe Dar na Habel Chidawali, Dodoma


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA