
Mradi wa Vitabu vya Watoto nchini (CBP), umeandaa tuzo kwa watoto na vijana kwa lengo la kuhamasisha uandishi wa kubuni vitabu kwa lugha ya Kiingereza.
Tuzo hiyo inayojulikana kama `Burt' imelenga kuondokana na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa vitabu bora vya kujisomea kwa watoto na vijana.
Katibu Mtendaji wa CBP, Pili Dumea, alisema jijini Dar es Salaam juzi kuwa wameamua kuandaa tuzo hiyo ili kuziba pengo la upungufu wa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza katika shule na maktaba mbalimbali nchini na kuboresha upatikanaji wake.
"Kumekuwa na upungufu wa vitabu vingi vya watoto na vijana katika maktaba zetu, hivyo tumeamua kuanzisha shindano la kuwashindanisha ili kupata vile ambavyo tunaweza kuvichapisha na kuvisambaza kwa vijana wetu," alisema.
Dumea alisema kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kutofahamu vyema lugha ya Kiingereza kwa ufasaha kutokana na kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili katika shule za msingi.
Alisema hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kuelewa lugha ya Kiingereza.
Alisema tuzo hiyo inalenga kuhamasisha zaidi watoto na vijana kubuni riwaya na hadithi kwa kuandika kwa lugha ya Kiingereza ili kuamsha shauku na kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha hiyo.
Dumea alisema lengo lingine la kutoa tuzo hiyo ni kuongeza vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza ili kuongeza vitabu katika maktaba na kuchangamsha tasnia ya uchapishaji.
Alisema mwisho wa kuwasilisha shindano hilo ni Machi 23, mwaka 2010 ambapo mshindi atatangazwa Julai Mosi, mwaka 2010.
Alifafanua kuwa mshindi wa shindano hilo atapewa dola 1,500 za Marekani.
0 comments:
Post a Comment