Rais Jakaya Kikwete ameutaka Umoja wa Mataifa (UN) kuheshimu na kuyatambua maamuzi yanayotolewa na kupitishwa na viongozi wa Afrika kupitia Umoja wa Afrika (AU) wa kutozitambua serikali zinazoingia madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia.
Kikwete alisema kama Umoja wa Mataifa utafanya kinyume na maazimio yanayopitishwa na viongozi hao wa kutozitambua na kuziondoa katika uanachama wa AU serikali zisizo halali itakuwa ni kufifisha mchakato wa ujenzi wa msingi ya demokrasiana utawala bora barani Afrika.
Kauli hiyo ya rais Kikwete uliwafanya wajumbe waliokuwa wakifuatilia hotuba yake katika ukumbi wa mikutano wa Baraza hilo, kupiga makofi ikiwa ni ishara ya kukubaliana na kile alichokuwa akikizungumzia.
Akihutubia mkutano wa 64 wa Baraza Kuu la UN, Kikwete alisema katika miaka michache iliyopita, Bara la Afrika limejikuta likikumbwa na jimamizi la mapinduzi ya kijeshi aliyoyataja kuwa hayafuati wala kuendana na misingi ya demokrasia.
“Afrika imekumbwa na jimamizi la mabadiliko yasiyofuata misingi ya kidemokrasia kwa kupitia mageuzi ya kijeshi na kile kinachoitwa nguvu ya umma zinazoshabikiwa na wanasiasa wafitini. Hawa wote wanataka kuingia madarakani kwa kutumia njia za mkato,” alisema na kuongeza:
“Umoja wa Afrika umejiwekea msingi na misimamo madhubuti na ambayo imo ndani ya Katiba yake wa kutozitambua serikali za aina hiyo na tumezisimamisha uanachama wa umoja wetu hadi hapo zitakaporejesha utawala wa kidemokrasia.”
Alisema maamuzi hayo ya UA yatakuwa na manufaa zaidi kama yataungwa mkono na Jumuia za Kimataifa na husani Umoja wa Mataifa.
Mambo mengine aliyoyazungumzia katika hotuba yake hiyo ni pamoja na suala la Palestine na Sahara ya Mgharibi.
Kwa upande wa suala la Palestine, Kikwete alisema anaunga mkono hoja ya kuwapo kwa mataifa mawili yaani lile la Paletine na Waisrael wakiishi kwa pamoja na kusisitiza kuwa Tanzania inaamini hilo ndio suluhisho pekee la kuleta amani ya kudumu katika Mashariki ya kati.
Kuhusu Sahara ya Magharibi, alisema suala la eneo hilo limekuwa likizungumzwa tangu mwaka 1975 na kwa sababu hiyo, akalitaka Baraza hilo kuharakisha mchakato wa kuwapatia raia wake fursa ya kujiamulia mambo yao.
0 comments:
Post a Comment