.jpg)
Tarehe 09.09.09 nusura iwe siku ya maafa makubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kama mabomu 14 ya kulipua vifaru yaliyokuwa yemepelekwa kiwanda cha nondo cha Simba Steel kama chuma chakavu yangetumika bila kubainika.
Mabomu hayo ni kati ya mzigo wa mabomu ya kijeshi 15 ya kulipua vifaru ambayo yalisafirishwa kutoka Zanzibar kwa majahazi, kisha kusafirishwa kwa lori hadi kiwandani hapo.
Aidha, moja kati ya mabomu hayo, lililipuka na kumjeruhi Bushiri Idd ambaye alikuwa utingo wa lori lenye namba za usajili T 818 AHX aina ya Leyland lililotumika kubeba mabomu hayo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi kiwandani hapo eneo la Mabibo Relini.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya asubuhi na kwamba watu watatu wanahojiwa, ikiwa ni siku mbili tu kabla ya dunia kukumbuka tukio la kigaidi baya kuliko yote yaliyotokea katika karne hii baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani.
Ingawa polisi hadi sasa hawajahusisha tukio la mabomu hayo na jaribio lolote la ugaidi, kugundulika kwa shehena kubwa kiasi hicho ya mabomu hatari tena yakipelekwa kiwandani, inaamsha hisia kama kuna uhusiano na tarehe la tukio la Septemba 11, ambalo miji ya New York na Washington ya Marekani, ilishambuliwa kwa ndege zilizotegwa na kugeuzwa silala za maangamzi.
Ndege hizo, mbili ziligongeshwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC) na nyingine makao makuu ya Jeshi la Marekani, Pentagon, ilihali nyimngine ikitunguliwa huko Pennsylvania.
Akisimulia tukio la Dar es Salaam, Kamanda Kova alisema Idd alijeruhiwa kifuani na moja ya mabomu hayo wakati akifanya usafi kwenye bodi ya gari hilo.
Alisema maafa hayo yalitokea eneo la Goodshed barabara ya Nyerere, Wilaya ya Temeke, wakati akifanya usafi kwenye gari hilo.
"Tulipata taarifa za kulipuka kwa bomu hilo, ambalo licha ya kusababisha majeruhi, lilileta uharibifu wa malori mawili yaliyokuwa yameengeshwa sehemu moja, lakini kitaalam bomu hilo halikulipuka lote, lingelipuka lote lingeleta maafa makubwa eneo hilo," alisema Kamanda Kova.
Alilitaja lori la pili kuwa ni lenye namba za usajili T 344 ADM.
Alisema kutokana na ukubwa wa tukio hilo, timu ya askari na maafisa wa kitengo cha uchunguzi wa kisayansi wa polisi pamoja na wataalam wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ilianza ufuatiliaji mara moja.
Alisema katika ufuatiliaji wao, walibaini kuwa aina ya mabomu ni anti-tank ambayo yanatumika kulipulia vifaru.
Alisema baada ya wataalam hao kupata taarifa nzima ya mzigo huo wa vyuma chakavu, waliamua kufuatilia zaidi katika kiwanda cha Simba Steel vilipopelekwa.
Alisema wataalam hao baada ya uchunguzi ndani ya kiwanda hicho walibaini kuwepo kwa mabomu mengine 14 yakiwa hayajalipuka.
"Mabomu haya ni hatari sana endapo yangelipuka ndani ya kiwanda hicho yangeleta maafa makubwa," alisema.
Kamanda Kova alisema timu hiyo ilimhoji dereva wa gari hilo, Nassoro Shaban (40), mkazi wa Temeke Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam ambaye alieleza kuwa alipata tenda ya kubeba vyuma hivyo kutoka kwa mtu aliyemtaja kwa jina moja la Hamis.
Alisema tenda hiyo aliipata Jumatatu ya wiki hii kutoka kwa mtu huyo na alimtaka avichukue kutoka bandarini na kuvipeleka kiwandani hapo.
Alisema dereva huyo baada ya kuvipakia vyuma hivyo siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni Jumanne, alivipeleka moja kwa moja kiwandani hapo kama alivyoagizwa na kulipwa ujira wake.
Kamanda Kova alisema dereva huyo alieleza kuwa baada ya kuvishusha vyuma hivyo, kiroba kimoja kilichokuwa na chuma chakavu kilisahaulika na alipelekea kwenye eneo la maegesho ya gari huko Goodshed, katika barabara ya Nyerere, bomu hilo lililipuka wakati utingo akifanya usafi wa gari.
"Sasa wakati utingo wake akifanya usafi ndipo moja ya bomu lililokuwa limesalia likalipuka na kumjeruhi," alisema.
Aidha, alisema katika uchunguzi wa awali aliofanya na timu hiyo, umebaini kuwa, mzigo huo ulitolewa Zanzibar na ulisafirishwa kuja bandari ya jijini Dar es Salaam kwa jahazi.
"Tumeelezwa kuwa huu mzigo uliletwa bandarini ukiwa umefungwa kwenye viroba kwa mafungu," alisema.
Kamanda Kova alisema uchunguzi dhidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kama kweli mzigo huo ulitoka Zanzibar au la.
Aidha alisema kuanzia sasa yeyote atakayekutwa na bomu/mabomu yakiwa kama vyuma chakavu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na watu wanaofanya biashara hiyo kutofuata sheria za usafirishaji wa vyuma hivyo.
"Sheria inasema kabla ya kusafirisha mzigo wa vyuma chakavu lazima mzigo ufanyiwe ukaguzi na wataalam ili kama kuna bomu au kitu hatari kiweze kuondolewa kabla ya kuleta madhara, lakini watu wamekuwa wakikiuka sheria na kusafirisha mizigo hii kiholela, matokeo yake ndio haya mtu analipuliwa na bomu," alisema.
Alisema kwa sasa mabomu hayo yamepelekwa jeshini Lugalo kwa uchunguzi zaidi ili kubaini kama yametoka nchini au nje ya nchi.
Alipotakiwa kueleza mabomu hayo yametoka nchi gani, Kamanda Kova alisema ilikuwa ngumu kufahamika kwa vile maandishi yaliyokuwemo kwenye mabomu hayo yalikuwa hayasomeki vizuri kutokana na kuchakaa.
0 comments:
Post a Comment