.jpg)
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana alikutana kwa mazungumzo ya faragha na Rais Dk. H. Susilo Bambang Yudhoyono wa Indonesia katika siku yake ya pili ya ziara ya siku tatu ya nchi hiyo.
Baada ya mazungumzo hayo, Waziri Mkuu Pinda na ujumbe wake, alitembelea mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji cha mpunga katika eneo la Ciberes, kilomita zaidi ya 150 kutoka Jakarta, mji mkuu wa Indonesia.
Vile vile, alitembelea kituo cha utafiti wa zao la mpunga cha Sukamandi ambapo aliambiwa wanasayansi wameweza kupata mbegu inayokomaa kwa siku 110 na hivyo inapandwa na kupata mavuno mara tatu kwa mwaka kwa kilimo cha umwagiliaji.
Baadhi ya wajumbe katika msafara huo pia walitembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza mbolea ya Urea na Amonia chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 900 za mbolea hizo kwa mwaka, ambapo malighafi yake kuu ni gesi asilia ya ardhini.
Lengo kuu la ziara ya Waziri Mkuu Indonesia ni kujifunza mafanikio makubwa ya kuendeleza kilimo yaliyopatikana katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia. Kabla ya Indonesia, Waziri Mkuu alimaliza ziara ya siku tatu ya Korea Kusini kwa madhumuni hayo hayo ya kilimo. Baadaye atakwenda India kabla ya kurudi nyumbani Septemba 18.
Waziri Mkuu anafuatana na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Mazingira wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Burhan Saadat Haji na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Iddi.
Vile vile, anafuatana na Wakuu wawili wa Mikoa, Luteni – Kanali mstaafu Issa Machibya wa Morogoro na Daniel Ole Njoolay wa Rukwa.
Wengine ni wataalamu wawili wa kilimo - Mkurugenzi wa Kikimo cha Umwagiliaji Maji, Mbogo Futakamba na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni binafsi ya mbegu na zana za kilimo ya Highland Seed Growers Ltd. ya Mbeya, Justin Mwiga.
Tanzania sasa inatekeleza mpango wa kuendeleza kasi ya kilimo, chini ya azma ya “Kilimo Kwanza” ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini kwa kutumia teknolojia na zana za kisasa, badala ya jembe la mkono.
0 comments:
Post a Comment