Ajali za barabarani zaua watu 1,400 mwaka huu
Jumla ya watu 1,468 wamepoteza maisha na wengine 8,373 kujeruhiwa vibaya katika ajali za barabarani nchini kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.
Jeshi la polisi kwa ushirikiano na watalamu kutoka Wizara ya miundombinu na Shirika la Viwango nchini, TBS, wamegundua vyanzo vikuu vya ajali hizo na kutoa mapendekezo ya namna ya kuziepuka ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaokufa kila leo pasi na hatia yoyote.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani, James Kombe, amesema utafiti huo umebaini kuwa madereva wengi huendesha gari kwa mwendo kasi na pia kufanya uzembe unaozaa ajali za mara kwa mara.
Sababu nyingine imetajwa kuwa ni kujaza mizigo zaidi ya uwezo wa gari, kutumia matairi chakavu na yasiyokuwa na viwango na baadhi ya mabasi kutengenezwa kwa chesesi za malori, kinyume na matakwa ya kiufundi, usalama na sheria.
Kombe akasema makosa hayo yameonekana kuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani na hivyo kusababisha ajali mbaya zinazopoteza maish aya Watanzania wasio na hatia.
"Hivi sasa tumejipanga na tunataka kudhibiti ajali zote zinazotokana na uzembe au baadhi ya watu kukiuka kanuni na sheria za usalama barabarani," akasema Kombe.
Akifafanua zaidi, akasema kwa kuanzia, madereva wote watapigwa msasa wa juu ya athari za mwendo wa kasi sana barabarani na athari zake, ikiwa ni pamoja na kuwapa takwimu za watu waliokufa kutokana na ajali hizo.
Akasema kuanzia sasa, gari zote zitakuwa na daftari maalum lenye kuonyesha muda wa gari kuondoka na kufika kwa kila mkoa na kwamba askari watakuwapo kwa kila kituo cha basi kwa ajili ya kusaini kitabu hicho.
"Tunaanza ukaguzi mkali kwa magari yote ya abiria... yale yaliyoungwa chesesi katikakati hayataruhusiwa kupakia abiria kabisa na mengine yalioungwa sehemu za mbele na nyuma yamepewa mwaka mmoja kubadilishwa," akasema Kamanda Kombe.
Akaongeza kuwa sasa wameona wazuie magari ambayo yameungwa chesesi kienyeji zaidi kwa kuwa yapo katika hatari ya kusababisha ajali zaidi kuliko yale yaliyoungwa mbele na nyuma tu.
0 comments:
Post a Comment