.jpg)
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana iliambiwa kwamba Sh. bilioni 3.8 za Akaunti ya Malipo ya Nje (Epa) katika Benki Kuu Tanzania (BoT), zilipitishwa kwa idhini ya mshitakiwa wa nne Imani Mwakosya kutoka katika benki hiyo na kuingizwa katika akaunti ya Mibale Farm.
Madai hayo yalitolewa jana na Mkuu wa Uendeshaji, Ronald Manongi (50) wa Commercial Bank of Africa (CBA) (zamani United Bank of Africa (UBA) wakati akitoa ushahidi mbele ya jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Mwenyekiti Samuel Karua, Beatrice Mutungi na Ilvin Mugeta wanaosikiliza kesi hiyo.
Upande wa mashitaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Boniface Stanslaus akisaidiana na Fredrick Manyanda.
Akiongozwa na Stanslaus, shahidi huyo alidai kuwa alipitisha fomu za kufungua akaunti ya kampuni ya Mibale Farm, ambapo walifungua akaunti namba 0101316004 katika benki hiyo.
Manongi alidai kuwa mwaka 2005, benki hiyo ilikuwa inatumia jina na UBA ambapo Novemba 3, mwaka huo, benki yake ilipokea ujumbe wa kibenki kutoka BoT ikieleza kwamba zimeingizwa fedha kwenye akaunti ya kampuni ya Mibale Farm.
Alidai kuwa katika ujumbe ulitoka BoT, Sh. 3,868,805,737.13 zilipitishwa na kuidhinishwa na mshtakiwa wa nne Mwakosya.
Mahakama iliahirisha kusikiliza kesi hiyo hadi leo baada ya shahidi wa pili upande wa mashitaka kutoweka mahakamani hapo.
Mbali na Mwakosya washtakiwa wengine ni Farijala Hussein, Rajabu Maranda, Ajay Somani, watumishi wa BoT, Esther Komu na Sofia Joseph.
Washtakiwa wanadaiwa kula njama ya kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu kutoka BoT, kwa kutumia kampuni ya kughushi ya Mibare Farm.
0 comments:
Post a Comment