.jpg)
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Mkoa wa Arusha limewaua kwa kuwapiga risasi watuhumiwa wawili wa uporaji wa Sh. milioni 61 katika Benki ya NMB Temeke jijini Dar es Salaam na kuwatia mbaroni wengine 11.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova watuhumiwa hao waliuawa kwa nyakati tofauti wakati wakirushiana risasi na polisi .
Kova, aliwataja watuhumiwa hao waliouawa kuwa ni Mussa Abdallah Mpemba (30), mkazi wa Yombo Buza maarufu kwa jina la Obadia Gabriel ambaye inadaiwa alisuka mipango ya wizi huo uliotokea mwezi uliopita katika benki hiyo.
Alisema mtuhumiwa huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi jijini Dar es Salaam alipokuwa akirushiana nao risasi wakati wakitaka kumkamata na huku akitumia silaha aina ya Walter.
Kova alimtaja mtuhumiwa mwingine aliyeuawa kwa kupigwa risasi mkoani Arusha kuwa ni Obadia Mwakihola (23) maarufu kama Kiburu mkazi wa Arusha.
Aliwataja watuhumiwa wengine wanaowashikilia ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kuwa ni Anthony Solia (30) maarufu kama Hamis Matonya, mkazi wa Dodoma.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa mjini Dodoma akiwa na magari matano kati ya manane yaliyokamatwa na polisi ambayo inadaiwa yalitumika katika tukio hilo la uporaji.
Alisema magari hayo yanafanyiwa utaratibu kuletwa jijini Dar es Salaam." Mpaka sasa magari mawili kati ya hayo yameshawasili jijini Dar es Salaam," alisema.
Awataja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Issack Swai (23), maarufu kama Bushoke au Fataki, mkazi wa Mtaa wa Moshi jijini Dar es Salaam, dereva, Deogratias Masawe (30), mkazi wa mtaa wa Mbuyuni, Moshi.
Wengine ni Salum Sule (28), maarufu kama Jibaba, mkazi wa Dar es Salaam, Yusuph Rajabu (44), mkazi wa Mbagala Mwanamtoti, Boniface Joseph (34), Japo Salimu (27), wakazi wa Yombo Dovya na dereva teksi, Said Hamisi (30), mkazi wa Tandika.
Alisema watuhumiwa wawili ambao majina yao hayajatajwa bado wanaendelea kuhojiwa.
Alisema kati yao, mmoja alikamatwa Kigoma na anadaiwa wakati wa tukio hilo alikuwa na mabomu na mwingine alikamatwa Arusha.
Alisema kati ya watuhumiwa hao, yupo askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Mgulani , mkazi wa Kibaha kwa Mathias mkoani Pwani.
Watuhumiwa wengine walikamatwa mkoani Mwanza na Kilimanjaro.
0 comments:
Post a Comment