Majambazi sugu, silaha, magari yanaswa katika msako
Msako ulioendeshwa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, umeweza kuwanasa majambazi sugu 7, silaha za kivita 4, magari 5 na vitu mbalimbali yalivyoporwa kwa wananchi.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana Kamanda Zelothe, alisema msako huo ulianza Julai Mosi hadi Julai 12 mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma na ulihusisha wahalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha, wavunjaji, wezi wa mifugo, matapeli, wabakaji na watuhumiwa wa makosa mbalimbali.
Aliwataja majambazi hao sugu waliokamatwa katika msako huo kuwa ni Oscar Juma au Abdallah Juma (20), Gau Salumu (32), Ahmed Maafuru (19), Hashim Jumanne (24), Jimmy Allen (24) na Abdallah Yusuph (28).
Alisema katika msako huo Polisi lilifanikiwa kukamata silaha ya kivita aina ya SMG yenye namba NM-18-1739 iliyokuwa imekatwa kitako na mtutu ambayo ilikuwa inatumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani Dodoma.
Alisema, silaha nyingine zilizokamatwa ni Shotgun moja iliyoporwa eneo la Dodoma Makulu, magobore matatu ambayo yaliporwa kwa walinzi waliokuwa lindo katika matukio mawili ya ujambazi na magobore mengine manane yalikamatwa wilayani Mpwapwa katika misako kama hiyo.
Alifafanua kuwa, katika msako huo jeshi hilo pia lilifanikiwa kukamata risasi za aina mbalimbali na makasha kadhaa ya baruti.
Kamanda Zelothe pia alisema, katika msako huo walifanikiwa kukamata magari matano ya wizi.
Magari hayo yalikamatwa kwa mtuhumiwa sugu wa ujambazi anayetumia majina matatu tofauti ya Hamis Bwashee, au Hamis Matonya au Antony Jeremia ambaye alifanikiwa kutoroka katika msako huo na bado wanaendelea kumsaka.
Zelothe alisema, msako huo pia uliekelezwa kwa wavutaji na wauzaji wa bangi, mirungi na gongo ambapo jumla ya watuhumiwa 49 walikamatwa wakiwa na misokoto 12,828 ambayo ni sawa na kilo 6.414 za bangi.
Pia walikamata watuhumiwa wengine 40 kati yao watatu walikamatwa na Cocaine gramu 25 na wawili walikamatwa na Heroine gramu 150, lita 142 za gongo na watuhumiwa 27 bado wanashikiliwa kwa matukio hayo.
Alizitaja mali zingine zilizokamatwa katika msako huo kuwa ni pamoja na pikipiki, televisheni, radio system, kompyuta na fedha bandia zenye thamani ya shilingi 310,000.
0 comments:
Post a Comment