
Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo, amejitosa rasmi kuwatetea watuhumiwa wa ufisadi na kumbeza Spika wa Bunge Samwel Sitta, kuwa anapoteza bure muda wa Bunge kujadili mambo yasiyo na maana kama kashfa ya Richmond.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, aliwashangaa watu wanaotaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) Dk. Edward Hoseah ajiuzulu wadhifa huo.
"Kwanza kabisa kuendelea kujadili suala hili ni kupoteza bure muda wa Bunge. Suala la Richmond limeshamalizika, nashangaa watu wanaoendelea kung'ang'ania, kila siku Richmond...Richomnd.... ni kupoteza muda, badala ya kujadili mambo ya maana tunajadili jambo ambalo halina maana kwetu, nataka hiyo Novemba suala hili liishe. Nataka Spika alihitimishe, tusigeuze Bunge sehemu ya kujadili mambo yasiyo na tija," alisema.
Hata hivyo, Cheyo alisema kwa upande wake yeye anaona kuwa tayari suala hilo limeshamalizika kwani hatua zimeshachukuliwa.
Alisema msimamo wa UDP ni kwamba baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu na kufuatiwa na Mawaziri Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, basi suala hilo ilibidi liishie hapo.
Alisema hakuna sababu tena ya Bunge kutoa azimio kwamba Hosea na Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali Johnsona Mwanyika wajiuluzu. "Hosea na Mwanyika hawawezi kujiuzulu au kuondoka madarakani kwa azimio la Bunge, wale sio wanasiasa. Wale hawakuwekwa na Bunge, bali wamewekwa na sheria iliyotungwa na Bunge, sasa kuanza kuwasakama kwamba wajiuzulu, ni kupoteza muda wa Bunge na kujaribu kulifanya Bunge liingie hadi jikoni kwa mambo yasiyo na msingi," alisema Cheyo.
Alidai kwamba licha ya kupoteza muda, masuala hayo (ya kuendelea kujadili Richmond) yanalishushia hadhi Bunge. Alisema suala la Richmond lilichukuliwa vema na likaisha, hivyo likiachwa liendelee itakuwa sawa na kuongeza maji kwenye mchuzi ambao tayari umeshaepuliwa jikoni.
"Tatizo la nchi hii ni kwamba watu wanapenda sana kuzungumzia issues (mambo) badala ya kuzungumzua issue (jambo), na mimi natoa onyo kuendelea kuzungumza sijui Richmond, sijui Hosea na Mwanyika wajiuzulu, tutaharibu mchuzi kweli nasema sitanii," alisema.
Alipoulizwa kwa nini hakutoa hoja hiyo kwenye Bunge lililopita, Cheyo alikuja juu na kusema katika mkutano huo (wa jana) alikuwa anatoa msimamo wa UDP na sio kama mbunge. "Kwani umeitwa hapa na mbunge au umeitwa na UDP, siwezi kuzungumzia mambo ya UDP bungeni," alisema.
Katika mkutano wa Bunge wa 16 uliomalizika Agosti mosi, mwaka huu, Bunge lilisitisha kujadili taarifa ya serikali ya utekelezaji wa maazimio kadhaa yanayoitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa serikali waliozembea na kuisababishia hasara serikali kwa kuipa kampuni ya mfukoni ya Richmond LLC ya Marekani zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa megawati 100 kwa thamani ya Sh. takribani bilioni 200 wakati kampuni hiyo ikiwa haina uwezo.
Katika hatua ya kushangaza, Cheyo alisema suala la ufisadi, limekuwa kama 'kawimbo' katamu, ambako waimbaji hawajui maana yake na kwamba haoni kama nchini kuna mtu ambaye siye fisadi.
Alisema hata wanasiasa wanaosema kuwa wanapinga ufisadi, ukiwachunguza utakuta nao ni mafisadi. "Hivi sasa watu wanafikiri kuwa na mapesa mengi ndio ufisadi, imefika mahali sasa naona neno 'fisadi' ni kama fahari fulani na umaarufu, kwani wanaopiga vita hawajui maana yake... wanaongea tu. Lakini ukiwauliza hasa hawawezi kukujibu kwa vile ni suala la kufikirika, ambalo halina maana, ni kama nilivyosema kuwa nchi hii watu wanapenda zaidi kuzungumzia issues badala ya issue," alisema.
0 comments:
Post a Comment