
Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustine Ramadhani, amesema mawakili nchini wanastahili kubeba lawama za baadhi ya kesi kuchelewa.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano mkuu wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika Law Society (TLS) uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mkuu alisema si kweli kwamba tatizo la ucheleweshwaji wa kesi linasababishwa na mahakama pekee, bali wanasheria nao husababisha matatizo hayo.
Alitolea mfano jinsi mawakili wanavyoweza kukata rufaa kwenye mahakama za juu, kutaka Jaji atamke kwamba mteja wake hana kesi ya kujibu.
"Utakuta kesi ipo Mahakama ya Wilaya au Mkoa, wakili anatoa hoja kwamba kwa hati ya mashtaka ilivyo na mazingira yanayodaiwa mteja wake kutenda kosa, inaonekana wazi mshitakiwa hana kesi ya kujibu.
Mahakama ikikataa wakili anakata rufaa mahakama kuu, huko nako ombi lake likikataliwa anakata rufaa Mahakama ya rufaa. Sasa hapa unaweza kuona muda unaopotea bure, wakati hata kesi yenyewe ya msingi inakuwa haijaanza kusikilizwa," alisema.
Jaji Ramadhani alisema anawashauri wanasheria kuhakikisha kesi husika inasikilizwa na akishindwa ndipo akate rufaa.
Akizungumza changamoto za jumuiya ya Afrika Mashariki Jaji Ramadhani alisema suala la lugha ya Kiingereza ni changamoto kubwa kwa wanasheria wa Tanzania.Alisema Kiingereza bado ni tatizo kubwa hasa ikizingatiwa kuwa lugha kubwa kwa Tanzania ni Kiswahili.
"Sisi Watanzania tunazungumza Kingereza katika maeneo machache sana tofauti na wenzetu ambao huzungumza kimombo kwa kila kitu.
Utakuta hata sisi majaji kuna kesi katika mahakama kuu na Mahakama ya rufaa tunazisikiliza kwa Kiswahili. Kwa hiyo kwa vile tumeingia kwenye ushirikiano, naomba Kiingereza sasa tukifanyie kazi ili twende sambamba na wenzetu," alisema.
0 comments:
Post a Comment