
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Valentino Mokiwa, amemtaja mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa ni mbinafsi na anayetakiwa kutubu dhambi ili alirejee Kanisa.
Akizungumza katika Jumuiya ya Mtakatifu Marko Mbezi Msigani jijini Dar es Salaam juzi, Askofu Mokiwa alisema kauli ya mwanasiasa huyo mkongwe kuwashambulia maaskofu kutokana na Waraka wa Kanisa Katoliki, imeonyesha namna gani alivyo mbinafsi na kutotaka mabadiliko.
"Kingunge ni mbinafsi, lazima aelewe kanisa lina uwezo wa kufanya lolote na likawa, hivyo lazima aelewe maelezo yanayotolewa na maaskofu ni agizo toka kwa Mungu ambaye ndiye anayewaweka kuwaongoza watu," alisema Askofu Mokiwa.
Alisema kutokana na kauli za ubinafsi za mwanasiasa huyo, inaonyesha ni jinsi gani anavyotakiwa kwenda kutubu kanisani na kulirudia Kanisa baada ya kuliasi.
"Dini inapaswa kuheshimiwa na mtu yeyote, haitakiwi kusemwa vibaya pale inapotoa matamshi yake kama Kingunge anavyokurupuka na kuongelea kitu ambacho hakifahamu," alisema. Mokiwa alisema ili Kingunge asipingane na maagizo ya Mungu anatakiwa ajiunge na kanisa ili aelewe maono ni kitu gani, lakini kabla ya kulirejea kanisa anatakiwa atubu makosa yake kwanza.
"Ni wakati wa wazee kama yeye kustaafu kuliko kukaa madarakani kwa muda mrefu...Kanisa Katoliki limefanya vyema kuwaambia wanachi kutochagua wala rushwa na mafisadi, sasa kwanini Kingunge anapingana na ushauri huo, anapenda mafisadi na wala rushwa?” alihoji Mokiwa.
Alisema licha ya kuwa waraka ule ulitolewa na Kanisa Katoliki, lakini kama askofu anaona unafaa kutokana na serikali inayosimamia Tume ya Uchaguzi kutochukua hatua yoyote pale tume hiyo inapofanya makosa katika uchaguzi. "Iwapo tume ingekuwa safi, tusingekuwa tunasikia kelele za wizi wa kura ama kesi za wagombea kupinga matokeo...kiongozi anaweza kutoka chama chochote lakini akiwa msafi," alisema.
Hata hivyo, alisema kutokana na Kingunge kuishiwa kitu cha kuzungumza, anatakiwa kujiweka kando na kuachana na ubinafsi alionao. Katikati ya wiki, Kingunge aliibuka na kulitaka Kanisa Katoliki limuombe radhi kutokana na kumuita fisadi, huku akiwataka maaskofu kutubu.
0 comments:
Post a Comment