Kaimu
mkurugenzi wa biashara na masoko wa shirika la ndege la Air Tanzania,
Juma Boma (wa pili kulia) akipanda ndege mpya aina ya CRJ-200 katika
uwanja wa ndege Julius Nyerere muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda
uwanja wa ndege wakimataifa wa Songwe. Shirika hilo limeanza safari zake
kwenda Mbeya ambapo itaruka mara nne kwa wiki.
Abiria
wakiwa ndani ya ndege mpya ya Air Tanzania aina ya CRJ-200 muda mfipi
kabla ya kutua katika uwanja wa ndege wa Songwe wakitokea Dar es
Salaam.
ATCL yaanza safari za kwenda Mbeya
Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Jumatatu hii lilizindua
safari zake za kwenda Mbeya kupitia uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa
Songwe likitumia ndege yake mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 50 ya
Canada aina ya CRJ – 200.
Safari hiyo inayochukua kadri ya saa moja kutoka Dar es Salaam
kwenda Mbeya itakayofanyika siku nne kwa wiki; Jumatatu, Jumatano,
Ijumaa na Jumapili, ililakiwa na abiria na wafanyabiashara wanaosafiria
kutoka Mbeya kwenda katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi wa kihistoria uliofanyika katika uwanja
wa ndege wa kimataifa wa Songwe, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara/Masoko wa
shirika hilo Bw. Juma Boma alisema Air Tanzania imerudi kwa kishindo
katika mji ambao ni kitovu cha biashara kwa mikoa ya nyanda za juu
kusini na inayotumika kama njia ya kuiunganisha Tanzania na nchi za
Kusini mwa Afrika, ili kupunguza adha ya usafirina kuiunganisha sehemu
ya Kusini mwa Tanzania na mikoa mingine.
“Safari ya Air Tanzania kwenda Mbeya iliyosubiriwa kwa muda mrefu
imeanza rasmi leo hii. Kwa kutumia ndege yetu mpya, tunatoa usafiri wa
haraka na salama, tukiiunganisha Mbeya na mikoa mingine. Kwa saa moja
tu, abiria wetu wanauhakika wa kutua uwanja wa ndege wa Songwe kutokea
Dar es Salaam.
“Tumezingatia masuala yote ya kiuchumi ili kupanga nauli tuliyoanza
nayo ambayo ni kiasi cha shilingi 150,000 kwa tiketi ya kwenda na
shilingi 260,000 kwa tiketi ya kwenda na kurudi,” alisema,” Bw. Boma.
Alisema uzinduzi wa njia ya Mbeya ni sehemu ya utekelezaji wa
mpango mkakati madhubuti wa upanuzi wa shirika, ambao umelenga katika
kuzirejesha safari zote za ndani na za kimataifa na kufungua njia
nyingine mpya.
Boma alisema kuwa kutokana na mkakati wao ujulikanao kama go-green
utalipelekea shirika hilo la ndege la taifa kuongeza toleo jipya ya
ndege nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 78 mwishoni mwa mwezi
Mei mwaka huu, shirika hilo litaongeza idadi ya safari zake katika njia
zake kuu na kuongeza safari za kimataifa.
“Kupitia upanuzi wa safari zetu, abiria wetu watafurahia safari za
kila siku kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, ikiwa muda wa kuondokea
Dar ukiwa ni saa 11 jioni na kutokea Mwanza ni saa moja usiku. Tutakuwa
tukienda mwanza mara nne kwa wiki.
Tutakuwa pia tukisafiri kwenda Moroni nchini Comoro katika siku za
Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi. Vile vile tunatarajia kufungua
njia ya Tabora – Mpanda hivi karibuni,” alisema.
Alibainisha kuwa shirika hilo pia limeondoa baadhi ya adhabu
watozwazo abiria wanaoshindwa kutokea wakati wa safari na wale
wanaobadilisha ratiba ya safari zao, na kusema kuwa hii itawasaidia
abiria wao kutoingia gharama za ziada endapo watakumbana na dharura
mbali mbali kabla ya safari.
Mmoja kati ya abiria aliyesafiria katika ndege hiyo kwenda Mbeya,
Deogratius Nyanshile aliipongeza Air Tanzania kwa maamuzi yake na kutoa
wito kwa watanzania kuliunga mkono shirika kwa kusafiria na Air
Tanzania.
“Nawaasa wakazi wa mkoa wa Mbeya na kanda ya kusini kwa ujumla,
kuitumia fursa hii kikamilifu iliyotolewa na shirika la Ndege la Air
Tanzania,” alisema Nyanshile. Ndege hiyo ya taifa, ambayo ilisimamisha
huduma zake katika mkoa huo kwa sababu ya ubovu wa uwanja wa ndege wa
zamani wa Mbeya, imerejesha safari hizo baada ya kukamilika kwa ujenzi
wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.
Ikitumia ndege yake aina ya Bombardier Dash-8, ATCL kwa sasa
shirika hilo linasafiri katika zaidi ya sehemu naneTanzania ikiwa
ni pamoja na Mtwara, Mwanza,
Tabora,Kigoma, Dar es Salaam, Bujumbura, Mbeya na kwendaMoroni nchini
Comoro.
0 comments:
Post a Comment