Na Immaculate Kilulya.
Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Emmanuel Nchimbi amewasimamisha kazi maofisa watano wa polisi wanaodaiwa kuhusika na tuhuma za dawa za kulevya pamoja na kubambikiza kesi zisizo na dhamana wananchi kwa kuendekeza rushwa.
Pia ametoa likizo ya lazima ya mwezi mmoja kwa Kamishna Msaidizi wa Polisi Renatus Chalamila anayedaiwa kujipatia fedha kutokana na ajira za polisi na kisha kuwafukuza wanafunzi 95 wa mafunzo ya upolisi baada ya kubainika kutumia rushwa kupata nafasi hizo.
Waziri Nchimbi amesema maofisa hao wanadaiwa kuhusika na upotevu wa ushahidi wa kilo 1.9 za madawa ya kulevya aina ya Cocaine yaliyokamatwa mkoani Mbeya ambayo baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali yalibainika kuwa sukari na chumvi.
Adhabu hiyo inakwenda sambamba na kufunguliwa mashitaka ya kijeshi.
Waziri Nchimbi pia ameongelea kuhusiana na sakata la Afisa wa Polisi Paul Mng’ong’o kuingia hifadhi za Mbuga za wanyama Serengeti na kupanga njama ya kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo.
Hatua hiyo ni baada ya Waziri Nchimbi kuteua timu maalumu ya uchunguzi wa matukio hayo kama sehemu ya mpango mkakati wa kuongeza maadili na ufanisi kwa jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa kuanzia ngazi za mafunzo ya polisi.
0 comments:
Post a Comment