Mlinzi wa klabu ya Chelsea, John Terry, atazikosa mechi mbili msimu ujao
utakapoanza wa mechi za Ulaya, kufuatia adhabu ya UEFA kumzuia asicheze
katika mechi tatu. Tayari aliikosa fainali dhidi ya Bayern Munich, baada ya kuonyeshwa
kadi nyekundu katika mchezo wa nusu fainali, wakati Chelsea ilipopambana
na Barcelona.
Lakini UEFA sasa imeamua kumuongezea adhabu, kwa kumkataza kucheza katika mechi mbili zaidi.
Terry pia hatakuwepo katika mechi ya Kombe la
Super dhidi ya washindi wa ligi ya Europa, Atletico Madrid ya Uhispania,
itakayochezwa mwezi Agosti, na vile vile mechi ya kwanza ya Chelsea
katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa ligi ya klabu bingwa Ulaya.
Terry na Chelsea wana muda wa siku tatu kuamua ikiwa watakata rufaa au la kufuatia uamuzi huo.
Terry, mwenye umri wa miaka 31, alitolewa kadi
nyekundu na mwamuzi, kufuatia kushindilia goti lake dhidi ya mchezaji wa
Barca, Alexis Sanchez, pasipo hata mpira kuwa karibu, wakati Chelsea
ilikuwa tayari imefungwa bao 1-0 usiku huo.
Aliwaomba msamaha wenzake kwa kuwaletea fedheha.
Hata hivyo licha ya kuondolewa Terry katika
mechi hiyo, hatua hiyo haikuinyima Chelsea ushindi, kwani hatimaye
iliondoka kwa sare ya 2-2, na katika uwanja wa Nou Camp, waliibuka
washindi kwa jumla ya magoli 3-2.
Kisha baada ya hapo walipata ubingwa wao wa
kwanza katika fainali ya klabu bingwa, licha ya kuwakosa wachezaji
mahiri Terry, Ramires, Branislav Ivanovic na Raul Meireles. |
0 comments:
Post a Comment