TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Sunday, June 24, 2012

Madaktari msigome, igeni mfano huu - Padre Privatus Karugendo

1:38 PM
Hii ni nukuu nusu ya makala ya Padri Karugendo kutoka gazeti la Tanzania Daima (kusoma makala nzima, kubofya hapa).
---

Ninawaomba madaktari wetu waige mfano wa Daktari Prathap C Reddy, wa India aliyeanzisha Hospitali ya Appolo. Daktari huyu alisomea India na baadaye alienda kujiendeleza kusoma Uingereza na Marekani. Alifanya kazi huko kwa muda na baadaye kuamua kurudi India.

Aliporudi India, jirani yake alikuwa mgonjwa na alihitaji matibabu nje ya India. Daktari Prathap, alijitahidi kumsaidia jirani kwa uwezo wake aliokuwa nao, lakini kwa vile alikuwa hana vifaa vya kisasa na fedha hazikupatikana kumpeleka nje ya nchi jirani yake huyo alikufa.

Tukio hilo lilimsikitisha, maana yeye alikuwa na utaalamu wa kumtibu, lakini hakuwa na vifaa na hakuwa na fedha kumsaidia aende kutibiwa nchi za nje. Tukio hilo lilimsikitisha na kumsonenesha. Hicho ndicho kilimsukuma kuanzisha Hospitali za Appolo.

Leo hii hospitali hizi zinasifika India na nje ya India, ni hospitali ambazo zinafanya kazi ya kuyaokoa maisha ya watu wa India na watu wa mataifa mengine.

Daktari huyu mwanzilishi wa Appolo, aliwashawishi madaktari waliokuwa wakifanya kazi kwenye hospitali za serikali na kulipwa mshahara kidogo kuachana na kazi za serikali na kuunga naye kuanzisha hospitali nzuri zenye vifaa vya kisasa.

Pamoja na kuwashawishi madaktari wa ndani ya nchi, alitembea dunia nzima akiwashawishi madaktari wahindi waliokuwa wakifanya kazi Ulaya na Amerika, kurudi nyumbani kuokoa maisha ya wahindi wenzao.

Appolo ilianza mwaka wa 1983, ikiwa na vitanda 150. Leo hii ina vitanda zaidi ya elfu nane, na imewatibu wagonjwa zaidi milioni 26 kutoka nchi 120 na Tanzania ikiwemo. Appolo wana hospitali zaidi ya 53 India na nchi nyingine na Tanzania ikiwamo.

Nilipokwenda India mwanzoni mwa mwezi huu, niliambiwa kuna Hospitali ya Appolo jijini Dar es Salaam. Bado naisaka hospitali hii nikiipata nitawashauri madaktari wetu waende huko jijifunza namna ya kujiunga na kufanya kazi pamoja.

Alichokifanya daktari huyu ni kuwakusanya madaktari, kutafuta mikopo kutoka kwenye mabenki makubwa na kuanzisha hospitali nzuri yenye vifaa vya kisasa. Madaktari hawa sasa wana mishahara mizuri ambayo wasingeweza kuipata kule serikalini.

Wanatoa huduma nzuri kwa wagonjwa na maisha yao yameboreka.

Hili ndilo ombi langu kwa madaktari wetu. Badala ya kuendeleza migomo na kuyaweka maisha ya watu hatarini, ni bora wakaachana na serikali. Wajiunge pamoja na kuanzisha hospitali ya binafsi nzuri na yenye vifaa vya kisasa.

Kama benki zinawakopesha wafanyabiashara wengine, kwanini zisiwakopeshe madaktari wetu wanaotaka kujenga hospitali nzuri na zenye vifaa vya kisasa?

Ninajua kuna hospitali ya namna hii iliyoanzishwa na madaktari bingwa wa Muhimbili, ni wazi inajitahidi, lakini bado inasuasua kwa huduma na haina vifaa vya kisasa.

Mbaya zaidi ni kwamba madaktari bingwa bado wanaendelea kufanya kazi Muhimbili, wakitoka huko wamechoka, wanakuwa hawana nguvu za kuwahudumia wagonjwa kwenye hospitali hiyo ya binafsi. Dawa pekee ni kuacha kazi serikalini na kujiunga pamoja kuanzisha hospitali bora zaidi.

Nina imani serikali inayokataa kuwasiliza madaktari leo hii, serikali inayokaa kutoa fedha za kumaliza matatizo ya madaktari, itatoa fedha nyingi kuwalipia viongozi na watu mbali mbali watakaotibiwa kwenye hosptiali binafsi za madaktari wetu.

Migomo ni mizuri kushinikiza kudai haki, lakini wakati mwingine si dawa ya matatizo yote. Dawa pekee ni madaktari kuachana na serikali na kuanzisha hospitali nzuri ya binafsi.

Tanzania tuna madaktari wazuri na wenye sifa za juu nje ya nchi. Ukienda Botswana, Namibia, na nchi nyingine za Ulaya na Amerika, utawakuta madaktari mabingwa kutoka Tanzania.

Hawa wakipata mtu wa kuwashawishi na kuwahamasisha kurudi nyumbani,Tanzania tunaweza kuwa na hospitali nzuri ya Afrika ya Mashariki na Kati.

Source: http://www.wavuti.com/#ixzz1yhDnirgs

0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA