Muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba uandikwe upya.
Mtandao
wa Jinsia Tanzania tumeupokea uamuzi wa Bunge wa kusogeza mbele muda wa
kuujadili muswada wa sheria ya mapitio ya Katiba wa 2011 kwa masikitiko
makubwa.Uamuzi wa Bunge unaoitaka serikali kuufanyia marekebisho
muswada huo na kuutafsiri kwa Kiswahili ni wamsingi ingawa una
mapungufu. Tulitarajia kwamba Bunge lingeishauri waziwazi serikali
kuuondoa muswada huo Bungeni na kuanzisha mchakato shirikishi wa kutunga
muswada mpya.
Kwa
hiyo, tunaunga mkono msimamo wa wananchi wanaoitaka serikali kuandaa
muswada mpya unaozingatia maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi.
Tunapenda
kusisistiza msimamo wetu kwamba wananchi hawapaswi kutungiwa sheria ya
kuanzisha mchakato na mfumo wa kutunga katiba mpya na chombo chochote
kabla hawajajadiliana na kukubaliana juu ya dira, tunu na maadili ya
Taifa lao. Msingi wa madai yetu ni mapungufu makubwa yaliyomo kwenye
muswada wa marejeo ya katiba wa 2011 uliowasilishwa na serikali Bungeni
kwa hati ya dharura. Muswada huu ulitungwa na serikali kabla ya
kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa na ndio maana ulikuwa na kasoro nyingi
zisizokubalika na watu wengi waliopata wafursa ya kuusoma na kutoa
maoni yao.
Tunasisitiza
kwamba, mjadala wa kujenga muafaka wa kitaifa unapaswa kuutangulia
mchakato wa kisheria wa kutunga katiba mpya. Mjadala wa Kitaifa ndio
utakaoainisha: wigo wa uwakilishi wa makundi mbalimbali; sifa za wajumbe
wa mkutano wa kitaifa wa katiba na kazi zake; sifa za wajumbe wa tume
huru ya katiba na hadidu za rejea za tume hiyo; sifa za wajumbe wa Bunge
la Katiba, muundo na kazi zake; na utaratibu wa kuandaa na kusimamia kura ya maoni.
Ili
mjadala huo uwe na tija, wananchi wanahitaji muda wa kutosha wa
kujadiliana na kukubaliana kwanza juu ya dira, misingi ya kisiasa na
kiuchumi na maadili ya taifa lao. Vilevile serikali inahitaji muda wa
kutosha wa kukusanya maoni ya wananchi na kuyachambua kabla ya kuandaa
sheria ya kusimamia mchakato wa kutunga katiba mpya.
Kazi
ya kuandaa na kuratibu mjadala wa kitaifa inapaswa kufanywa na chombo
huru kinachoundwa na wataalamu wenye misimamo thabiti na sio vyombo au
taasisi za dola. Tunaitaka Serikali kuheshimu maamuzi ya wananchi
yatakayotolewa wakati wa mjadala huo. Tunasisitiza kwamba maamuzi ya wananchi ndiyo yatakayozaa sheria nzuri ya mchakato na mfumo wa kutunga katiba mpya.
Tunalitaka
Bunge kutimiza wajibu wake wakikatiba kwa kuishauri Serikali juu ya
namna bora ya kuandaa na kuratibu mjadala wa kitaifa ili wananchi wote
waweze kushiriki kwa amani,utulivu na kuvumiliana. Bunge linapaswa pia
kushirikiana na serikali katika kuweka mazingira muafaka ya kisiasa na
kisheria ili mchakato wa kutunga katiba ukamilike kwa mujibu wa
matarajio ya watanzania wote.
Tunawataka
wanasiasa wote kutambua wajibu wao wa kutetea maslahi ya taifa na
kuepuke kuweka mbele maslahi ya vyama vyao wanapowasilisha hoja zao
ndani na nje ya Bunge. Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia haki na
wajibu wao wa kuunda katiba mpya, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa
na wadau wote wa siasa nchini:
a) Kuafikiana juu ya mfumo wa kuratibu mjadala wa kitaifa utakaoweka misingi ya kisiasa na kisheria ya kutunga katiba mpya.
b) Kuafikiana
juu ya sheria ya kuunda Bunge la katiba na sheria ya kuandaa na
kusimamia kura ya maoni. Sheria hizi zitatungwa na Bunge kwa kuzingatia
mapendekezo ya wananchi yatakayotokana na mjadala ya kitaifa
ulioratibiwa na tume huru ya katiba.
c) Kushirikiana
kuweka mazingira muafaka ya kisiasa yatakayowezesha wananchi wote
kushiriki katika mchakato wa kutunga katiba mpya bila hofu au kuburuzwa
na kundi la watu au taasisi yoyote.
d) Bunge
kutotunga sheria yoyote yenye lengo au mwelekeo wa kuchakachua mchakato
wa kutunga katiba mpya katika kipindi chote cha mchakato wa kutunga
katiba mpya.
e) Kuafikiana juu ya muda wa mchakato wa kutunga katiba.
f) Kuafikiana juu ya namna ya kutoa elimu kwa wananchi wote ili waweze kushiriki ipasavyo katika mchakato wa kutunga katiba.
MJADALA KWANZA, SHERIA BAADAYE!
Imetolewa Dar es salaam na
Mary Rusimbi
Mwenyekiti wa Bodi TGNP
0 comments:
Post a Comment