Karibu
msomaji wangu. Uwanja wetu ni ule ule na maudhui ni yale yale, sisi
bado hatujajivua magamba. Inampendeza Mungu kila upande.
Mapenzi yana uwanja mpana ingawa sura zake ni mbili.
Amani kwa maana ya pale ambapo mambo yametulia na migogoro kwenye eneo ambalo wawili wanaopendana hawana furaha wala maelewano.
Mada hii itakuwa na lengo moja tu la kuponya wale wote wanaoishi kwenye
mapenzi yasiyo na amani. Yale yanayoashiria kifo cha mapema na kuwafanya
wabadili uelekeo.
Wanaweza kuanza kuheshimu kile kilichowaunganisha. Yaani kuufanya
‘uspesho’ wao uwe na maana. Ikiwa hivyo, basi watakuwa wanaondokana na
jinamizi la kifo cha haraka. Hapa si utani, inahitaji utulivu kujua.
Msongo wa mawazo kila siku au mara kwa mara, husababisha mwili kushindwa
kufanya kazi sawasawa. Athari kubwa huelekea kwenye moyo ambao ndiyo
injini ya mwili wa binadamu.
Mapenzi ndiyo kitu namba moja kinachoweza kumfanya mtu awe na msongo
mkubwa wa mawazo. Fedha au njia zake ni kichocheo namba mbili lakini
kina unafuu wake pale unapopata faraja kutoka kwa mwenzio.
Katika mapenzi hakuna kinachoweza kukupa ahueni zaidi ya kuelewana na
yule unayempenda. Yule aliyekuudhi, vinginevyo utakosa utulivu wako.
Mapenzi yanaua lakini sizungumzii kunywa sumu.
Nazungumzia athari inayojengeka katika moyo baada ya kutokuwa kwenye
maelewano chanya na mwenzi wako. Mwili unakosa upumuaji mzuri, hivyo
kutema sumu ndani kwa ndani. Matokeo yake unajiona mgonjwa, kumbe
mapenzi.
WAPO WATU WA AINA HII
Mtu hana maelewano na mwenzi wake, moyo unamlazimisha atafute suluhu
lakini anakuwa mbishi. Anataka kujionesha kwamba yeye yupo salama na
hatishiki kwa lolote.
Saikolojia inakutaka ujitunze usiumizwe. Yaani uwe na tahadhari kutafuta
suluhu pale isipostahili lakini kama ishu ni ndogo, iweje isiwekwe
mezani na kutafuta ufumbuzi?
Mara nyingi mtu huyu huumia sana baadaye hasa baada ya kugundua ukweli
kuwa yule aliyekuwa anamfanyia ‘ushenzi’ amekwishaondoka na pengine
hatarudi tena kwake. Amechezea mawe, kapoteza almasi lakini majuto
mjukuu!
WAPO NA HAWA
Ipo jamii ya watu ambao hutaka jamii iwaone wao ni ngangari katika
mapenzi. Yaani hawawezi kuumia hata wafanywe nini. Wanajidanganya kwa
‘ubishoo’ wao. Kuna kitu utajifunza leo.
Ukweli ni kuwa, hakuna mtu ambaye anaweza kujitenga na maumivu ya moyo
pale anapoumizwa na mtu anayempenda. Anaweza kutabasamu akiwa na wewe
lakini peke yake ni kilio cha ndani kwa ndani.
Yaani hayupo kwenye hali nzuri na mwenzi wake lakini eti anadhani
akisema atachekwa. Amekwishajiaminisha yeye ni ngangari lakini ikae
kichwani kuwa mtu wa aina hii ni rahisi kufa.
Si kwa kujinyonga isipokuwa anaweza kuangamia taratibu. Hapa nataka
nikupe pointi bora ya maisha kuwa, fanya kila uwezalo kuhakikisha moyo
wako unakuwa salama. Usiupe mzigo usio wa lazima.
Maumivu ya mara kwa mara ya kimapenzi ni mzigo mkubwa mno ambao
huutwisha moyo wako. Masikini ya Mungu, wenyewe huwa hausemi kwa kutoa
sauti ila unapoelemewa maumivu hukurudia mwenyewe.
HAWA NAO VIPI?
Wapo ambao huumizwa wao lakini kutwa kiguu na njia kutafuta suluhu.
Haikatazwi kwa maana anatafuta amani ya moyo wake lakini muhimu ni je,
huyo anayehangaikiwa yupo vipi?
Ni kujipa mzigo mzito kichwani kubembeleza penzi la mtu ambaye hana
hisia na wewe hata kidogo. Bora uumie leo, tafuta faraja kwa watu wako
wa karibu, omba kwa Mungu akuvushe salama katika kipindi kigumu.
Anakutenda leo, wewe ndiye unayepigana kutafuta amani irejee na upendo
uendelee. Binadamu alivyo na hulka ya ajabu, ukifanya hivyo hawezi
kukuona ni mtu bora, isipokuwa ataamini amekupata na huna ujanja, hivyo
atarudia yale yale.
Shukuru Mungu kwa namna alivyokuumba. Wewe ni kiumbe kamili, huna
upungufu wa aina yoyote, hivyo usikubali mtu mwingine aje auponde moyo
wako. Hata siku moja usiruhusu mtu acheze sebene na moyo wako.
Unatakiwa kuwa wa kwanza kujihurumia kwa sababu hayupo atakayehisi
maumivu kwa niaba yako. Kumruhusu mtu anayekuumiza mara kwa mara ni sawa
na kutonesha kidonda ambacho ni injini ya mwili wako. Moyo!
|
0 comments:
Post a Comment