Kikwete wakizungumza na wanafunzi wa shule ya
Sekondari ya wasichana WAMA Nakayama,iliyopo
Nyamisati,wilaya ya Rufiji wakati Rais Kikwete
alipokwenda kuikagua jana.
(Picha na Freddy Maro
wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya WAMA-
Nakayama iliyopo katika kijiji cha Nyamisati wilaya ya
Rufiji, Mkoa wa Pwani. Rais Kikwete aliitembelea na
kuikagua shule hiyo ya mfano ambayo inahudumia watoto
Yatima na wale wanaotoka familia maskini na mazingira
magumu wanaofadhiliwa na Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo WAMA inayoongozwa na
Mama Salma Kikwete
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Februari 10, 2011, ametembelea na kukagua Shule ya Sekondari ya Wama-Nakayama iliyoko Kijiji cha Nyamisati, Kata ya Salale, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Shule hiyo inayomilikiwa na kuendeshwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo mwenyekiti wake wa Bodi ni Mama Salma Kikwete, inatoa elimu ya sekondari bure bila malipo yoyote kwa watoto wa kike yatima, waliokulia katika maisha hatarishi na wale ambao wazazi wao hawana uwezo kabisa wa kuwasomesha watoto wao.
Katika maelezo yake kwa Mheshimiwa Rais, Katibu wa WAMA, Bwana Daudi Nasibu amesema kuwa shule hiyo iliyoanza kujengwa mwanzoni mwa mwaka 2008 kwa msaada wa kuanzia kutoka Taasisi ya Nakayama ya Japan sasa inao wanafunzi 82 ambao wako kidato cha pili na cha tatu. Wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka huu wataanza masomo keshokuwa, Jumamosi, Februari 12, mwaka huu.
Rais Kikwete ameambiwa kuwa ujenzi kwenye shule hiyo bado unaendelea na makusudio ni kuiwezesha shule hiyo kuwa na uwezo wa kuwa na wanafunzi 510 kwa wakati mmoja.
Bw. Nasibu amesema kuwa shule hiyo yenye walimu wanane chini ya Mwalimu Mkuu, Twaha A Twaha siyo tu kwamba inatoa elimu bure kwa wanafunzi lakini pia inalipia mahitaji yote ya wanafunzi ikiwa ni pamoja na nauli ya kuwasafirisha kutoka nyumbani hadi shule na kurejea makwao wakati wa likizo.
Bw. Nasibu pia amemweleza Mheshimiwa Rais baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maji na umeme wa kutosha, ukosefu wa zahanati na usafiri wa uhakika kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo iliyoko kiasi cha umbali wa kilomita 156 kutoka Dar Es Salaam, na umbali wa kilomita 42 kutoka kwenye Barabara Kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi.
Akisalimiana kwa ufupi tu na wanafunzi wa shule hiyo na wanakijiji cha Nyamisati waliofika shuleni hapo kumpokea na kumsikiliza, Rais Kikwete ameipongeza Bodi ya WAMA kwa wazo na uamuzi wa busara wa kujenga shule hiyo, akawapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi nzuri, na akawapongeza wanakijiji waliotoa ardhi ambako shule hiyo imejengwa.
Kwa wanafunzi, Rais amesema: “Nyie hamna tatizo la ada ya shule, hamna tatizo la nauli ya kuwafikisha shule, hamna tatizo la chakula. Katika hali hiyo mnabakia na ada moja: kusoma kwa bidii na uwezo wenu nyote,”
Ameongeza: “Kusoma kwa bidii sana ndilo tumaini letu. Ndiyo tumaini ya ndugu zenu kwa sababu nyie mkishakusoma mtasaidia kuwatoa ndugu zenu kwenye umasikini.”
Baadaye Rais Kikwete alisimama kwa muda kwenye bandari ndogo ya Nyamisati na kusikiliza kero za wananchi kwenye kijiji hicho. Rais amerejea Dar es Salaam leo jioni.
Mwisho.
Imetolewa na:
a ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Februari, 2011
0 comments:
Post a Comment