Waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro, wamepokea msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh. milioni 5, kutoka serikali ya watu wa China kupitia ubalozi wao nchini, kwa lengo la kuwasaidia kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii yanayowakabili, ikiwemo nishati ya umeme.
Mbunge wa jimbo hilo, Mustapha Mkulo, alisema kuwa amepokea vifaa hivyo kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, ikiwa ni misaada kutoka kwa serikali ya China, baada ya Rais huyo wa Tanzania na mabalozi wa nchi mbalimbali kutembelea wilaya hiyo na kujionea mafuriko yalivyoathiri jamii hiyo.
Aliitaja misaada mingine kuwa ni radio 1,500 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari zilizopo katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko wilayani humo, vituo vya elimu na baiskeli 80 kwa kila afisa mtendaji kata na afisa elimu kata, ambapo kila kata zitatolewa pikipiki mbili na zitakazobaki zitapelekwa makao makuu ya wilaya.
Mingine ni televisheni 15 kubwa kwa sekondari zilizopo maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, Chuo cha Ilonga, Chuo cha Maendeleo Ilonga, Chuo cha Vijana Ilonga, Chuo cha Ualimu Ilonga na Chuo cha Utafiti Ilonga, pamoja na televisheni ndogo 20 kwa ajili ya maeneo yaliyoathirika na mafuriko.
Misaada mingine ni jozi 3,600 za viatu (kandambili maarufu kwa jina la "yeboyebo" kwa wanafunzi wa sekondari maeneo yaliyoathirika na mafuriko, pamoja na jozi 360 za sapato (viatu vya kuchomeka) kwa wanafunzi wa kike kwa shule za sekondari zilizoathiriwa na mafuriko, mabati 554 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa waathirika, pamoja na vyerehani 50 kwa vikundi vya akina mama katika kata nane za wilaya ya Kilosa.
Vifaa vingine ni genereta tano za umeme wa upepo kwa ajili ya makambi yanayohifadhi watu ambao nyumba zao zimebomolewa na mafuriko, seti 20 za vyombo vya muziki kwa ajili ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, mashine za maji tano kwa ajili ya vituo vya afya, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 51.
0 comments:
Post a Comment