TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameondoka nchini leo, Jumatano, Februari 17, 2010, kwenda Uturuki na Jordan, kwa ziara rasmi za kiserikali kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hizo mbili.
Rais Kikwete ambaye anaandamana na Mama Salma Kikwete, pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania, anatarajiwa kuwasili Ankara, Uturuki, usiku huu tayari kuanza kwa ziara ya siku tatu nchini humu kwa mwaliko wa Mheshimiwa Rais Abdallah Gul.
Rais Kikwete alipokea na kukubali mwaliko wa kutembelea Uturuki tokea Februari mwaka jana wakati Mheshimiwa Rais Gul alipotembelea Tanzania kwa ziara ya pili kwa mwaliko wa Rais Kikwete.
Wakati wa ziara hiyo ya Uturuki, Rais Kikwete anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, na pia kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan.
Miongoni mwa shughuli zake wakati wa ziara hiyo, Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Uturuki, pamoja na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika Uturuki.
Tanzania na Uturuki zinatarajiwa kutiliana saini mikataba sita ya ushirikiano kati ya nchi hizo wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Kikwete.
Aidha, Rais Kikwete atatunukiwa shahada ya juu kabisa (PHD) ya heshima na Chuo Kikuu cha Faith cha Fatih cha mjini Istanbul.
Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka Uturuki Jumapili, Februari 21, 2010, kwenda Jordan kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa MfalmeAbdullah wa Pili.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Februari, 2009
0 comments:
Post a Comment