Ukosefu wa huduma ya umeme Zanzibar umeanza kuleta athari kubwa za kiuchumi ikiwemo viwanda kufungwa, kupanda kwa gharama za uendeshaji wa hoteli za kitalii na mamia ya wajasiriamali kupoteza kazi walizokuwa wakizifanya na kujipatia kipato.Uchunguzi wa Nipashe umegundua kuwa idadi kubwa ya watu waliokuwa wamejiajiri hasa katika viwanda vidogo vidogo vya uchongaji wa samani, kuchomelea vyuma pamoja na akinamama wanaotengeneza viburudisho baridi kama juisi na vyakula wamepoteza kazi.
Aidha, vijana waliokuwa wamejiajiri kwa kuanzisha maduka ya kunyoa nywele, idadi kubwa wamelazimika kufunga na kukaa vijiweni, wakati nyumba nyingi za kulala wageni zikishindwa kupokea wageni kutokana na ukosefu wa maji na umeme.
Wakala wa kusambaza vyakula katika hoteli za kitalii, Mussa Shauri, alisema kabla ya kukosekana umeme walikuwa wakisambaza vyakula vya milioni sita katika hoteli hizo.
“Wenye mahoteli ya kitalii wanaogopa kuchukua vyakula vingi kutokana na kukosa umeme wa uhakika, hasa kwa kuzingatia umeme wa jenareta ni tofauti na umeme wa kawaida,” alisema Shauri. Alisema binafsi amekuwa akipeleka vyakula katika hoteli za Venta Club, Palumbo na Verra, lakini tangu kukosekana kwa umeme biashara imekuwa ngumu.
Alisema samaki wanaowachukua sasa kutoka kwa wavuvi wanalazimika kwenda kuwahifadhi Tanzania Bara na baadaye kuwapeleka kidogo kidogo mahotelini kwa kutumia usafiri wa boti kila siku.
Hata hivyo, Shauri alisema kabla ya Serikali kupiga marufuku uingizaji wa barafu kutoka Tanzania Bara, walikuwa wakiwahifadhi samaki hao kwa kutumia mabarafu hayo, uamuzi ambao alisema umeathiri biashara hiyo.
“Tupo katika hatari ya kufilisika kama Serikali itaendelea na uamuzi wake wa kuzuia barafu kutoka Tanzania Bara kwa vile zilikuwa zikitusaidia kuendesha biashara licha ya soko kuwa dogo,” alisema Shauri. Kwa upande wake, Hoteli ya Serena Inn, inalazimika kutumia Sh. milioni 34 kwa mwezi kama gharama za mafuta, wakati ilikuwa ikitumia Sh. milioni 15 kwa mwezi kabla ya kukosekana kwa umeme.
“Hali ni mbaya na tunalazimika kutumia lita 960 za mafuta ya diezeli kwa siku hatuwezi kulaza wageni gizani,” alisema ofisa mmoja mwandamizi wa hoteli hiyo ambaye alikataa kutajwa jina lake.
Hoteli ya Mbweni Ruins iliyopo Mbweni Zanzibar imesema sasa inatumia Sh. milioni 12 kwa mwezi kama gharama za umeme kutoka Sh. milioni tatu kwa mwezi kabla ya tatizo la umeme, kama gharama za kuendeshea jenereta.
Hoteli ya Palumbo imesema hivi sasa inatumia Sh. milioni 1.2 kwa siku kama gharama za mafuta.
“Tatizo la umeme limetuathiri kwa vile tunatumia kiwango kikubwa cha fedha kununua mafuta na kwa kweli tunapata wakati mgumu,” alisema meneja wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Lucas.
Said Ali, mfanyabiashara katika soko la Darajani, alisema biashara yake ya nyama imeathirika na kwamba alikuwa akiuza kilo 100 kwa siku, lakini sasa anauza chini ya kilo 50.
“Ombi letu kwa Serikali ni kuwa itafute umeme wa dharura wakati matengenezo yakiendelea, kwa vile tunaendelea kuathirika kibiashara,” alisema mfanyabiashara huyo.
Mafundi ujenzi na useremala wamesema kazi zao zimeathirika vibaya kutokana na tatizo la uhaba wa maji na kupanda kwa gaharama za kuchonga vifaa kutokana na viwanda vingi vidogo vidogo kusitisha uzalishaji.
“Ubao mmoja hivi sasa kuuranda ni Sh. 2,000 badala ya Sh. 300 na viwanda vilivyobakia kufanya kazi hiyo ni vichache,” alisema Khamis Masoud, fundi seremala katika eneo la Mbweni na kuongeza kuwa kwa sasa kazi hiyo inafanyika katika kiwanda cha Amani pekee, lakini gharama ni kubwa.
Aidha viwanda viwili vya utengenezaji maji vimesitisha uzalishaji ikiwemo kiwanda cha Zainab Bottles kinachozalisha maji aina ya Kool na kiwanda cha Lootar Group Company kinachozalisha maji aina ya Drop, kutokana na ukosefu wa umeme.
Kutokana na viwanda hivyo kusitisha uzalishaji, maji pekee ambayo yanapatikana Zanzibar ni Kilimanjaro na Dasan, ambayo hutengenezwa Tanzania Bara.
Meneja Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Hassan Ali Mbarouk, alisema wafanyakazi wa shirika hilo wamelazimika kugeuka walinzi kutokana na kukosa kazi za kufanya.
“Wafanyakazi tumekuwa tukiwapangia kazi za ulinzi kulinda nyaya na transfoma kwa vile tayari kumejitokeza tatizo la wizi wa nyaya katika baadhi ya maeneo,” alisema Mbarouk.
Alisema Zeco linatarajia kupata hasara ya Sh. bilioni 2.2 kila mwezi, lakini mafundi wanaendelea na matengenezo na huduma hiyo inatarajiwa kurejea kuanzia Februari 20.
Nao wafanayabiashara ya kanga katika mtaa wa Mkunazini, wamesema biashara ya nguo imeathirika kwa vile wateja wao wakubwa ni akinamama wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo, ambao sasa wamezifunga kama za utengenezaji wa juisi, keki.
“Kwa siku nilikuwa nauza doti 20 za kanga hadi 30, lakini sasa biashara imekuwa ngumu kwa vile wateja wetu wakubwa ni wafanyabaishara wadogo wadogo hasa akinamama,” alisema Juma Khamis.
Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, alisema Serikali imekuwa ikitumia Sh. milioni 12 kwa siku kama gharama za mafuta katika vyanzo vya maji.
Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar imeamua kupeleka majenereta katika vyanzo vya maji ili kukabiliana na tatizo la upngufu wa maji.
“Hakuna ambaye hajaathirika na tatizo hili la maji, hata viongozi wa kitaifa na wastaafu wameathirika kwa tatizo hili,” alisema Waziri Mansour. Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji, Samia Suluhu Hassan, alisema viwanda vya kuzalisha maji Zanzibar vimeathirika pamoja na viwanda vidogo vidogo na kuathiri watu waliokuwa wakinufaika na sekta hiyo.
Hata hivyo, alisema watalii bado wanaendelea kwenda Zanzibar licha ya kujitokeza tatizo la umeme ingawa alisema ni kweli gharama za uendeshaji wa hoteli za kitalii zimeongezeka.
Katika mitaa ya Zanzibar watu wamekuwa wakigongana na mabegi ya nguo kila mmoja akitafuta sehemu ya kufua au kunyoosha nguo kwa dobi wanaotumia pasi za mkaa.
Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, alisema tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekwisha kumtaarifu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mizengo Pinda, kuhusu tatizo la umeme Zanzibar. Nahodha alisema amemwandikia barua Pinda kumtaarifu tatizo lilijitokeza huku Serikali ikiendelea kuchukuwa hatua mbalimbali za kurejesha huduma ya umeme Zanzibar.
Hata hivyo, Nahodha alisema Wazanzibari suala la kuomba bado wanaliona kama ni la aibu kwa vile suala hilo liko nje ya utamaduni wa Mzanzibari.
“Unapovunjika mguu huna haja ya kumuomba kaka yako akufanyie matibabu bali utamtumia salamu kuwa nimeumia, inatosha hiyo huna haja ya kumuomba yeye mwenyewe atafahamu,” alisema.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwa na subira kwa vile Serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, ikiwemo kuendelea na mpango wa kuwa na umeme wa dharura badala ya kutegemea chanzo kimoja cha umeme.
Wakati huo huo, kesi za ugonjwa wa kipindupindu zimeripotiwa kujitokeza katika kijiji cha Donge na Jambiani na zaidi ya watu 47 wameripotiwa kuugua.
Wananchi wamekuwa wakitakiwa kuchemsha maji kabla ya kuyatumia ili kujiepusha na maradhi ya milipuko hasa wakati huu wa upungufu wa maji kutokana na tatizo la umeme.
Biashara ya maji imekuwa kubwa katika Manispaa ya Zanzibar na ndoo moja inauzwa Sh. 500 badala ya Sh. 200 kabla ya kujitokeza kwa tatizo hilo.
Huduma ya umeme ilitoweka Zanzibar baada ya kifaa kinachopokea umeme katika kituo cha Fumba kulipuka Desemba 10, mwaka jana na kusababisha athari kubwa ya upatikanaji wa huduma za kijamii.
Hata hivyo waya unaopokea umeme kutoka Tanzania Bara umemaliza muda wake wa matumizi kwa miaka 30 na hiyo ni mara ya tatu kulipuka ambapo kwa mara ya kwanza ulilipuka Mei mwaka juzi na kusababisha wananchi kukosa huduma hiyo kwa mwezi mmoja.
0 comments:
Post a Comment