TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Wednesday, December 30, 2009

Polisi ampiga raia risasi Dar

3:33 PM
Mfanyabiashara wa milango na madirisha katika eneo la Tazara Veterinary almaarufu kama Mapambano jijini Dar es Salaam, Ally Sarange, amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi wakati akishuhudia kukamatwa kwa mtuhumiwa.
Wakizungumza katika eneo hilo, wafanyabiashara hao wamesema tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi wakati walipokuwa wakishuhudia kukamatwa kwa kijana mmoja.
“Tuliona askari watatu wakimfukuza mtu kutoka huko juu ikabidi tusogee kujua kulikoni na tulipofika karibu tulisikia akilalamika niacheni, niacheni, mtaniua,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Said Amiri.
Alisema baadaye mtu huyo alizidiwa mbio na polisi na kuamua kuketi chini karibu na lango la kuingia kiwanda cha ALAF huku akiendelea kuwataka polisi kumuachia.
Alisema mmoja wa polisi hao waliokuwa wamevalia kiraia alitoa pingu kumfunga kijana huyo mkono mmoja lakini wakati akitaka kumfunga mkono wa pili, aliwataka watu kusogea nyuma.
Alisema watu waliokuwa katika eneo hilo walitii amri hiyo na kusogea nyuma lakini walimuona askari mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Ngonyani alichomoa bastola kutoka katika suruali yake na kisha kufyatua risasi juu.
“Lakini wakati akishusha chini ile bastola, risasi ilichomoka na kumpiga mfanyabiashara mwenzetu katika mdomo na kuanza kuvuja damu,” alisema. Alisema mara baada ya kupigwa risasi hiyo mdomoni alivuja damu nyingi kabla ya kudondoka chini, hali ambayo iliwafanya watu waliokuwa wanashuhudia kufikiria kuwa amekufa.
Habari kutoka eneo hilo zilisema baada ya tukio hilo, wananchi waliwarushia mawe polisi hao, hali ambayo ilimfanya askari aliyempiga risasi mfanyabiashara huyo kujeruhiwa kichwani.
Mashuhuda hao walisema polisi hao walitimua mbio kwenda kujificha katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika kiwanda cha ALAF, hadi hapo polisi wenzao walipojitokeza na kuwaokoa.
Hata hivyo, majeruhi huyo alichukuliwa na mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo na kupelekwa katika Hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara walioambatana na Sarange alipewa rufaa kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji na kuondolewa risasi moja mdomoni.
Wafanyabiashara hao walisema majeruhi huyo amelazwa katika Wodi ya Sewahaji namba tano.
Habari kutoka katika eneo hilo, zinadai kuwa polisi hao walikuwa katika operesheni ya kuwasaka wavuta bangi katika soko la Tazara Veterinary.
“Hawa walimkamata kijana mmoja huko sokoni lakini wenzake wakawa wanakataa asikamatwe ndipo polisi hao walianza kumfukuza hadi karibu na kiwanda cha ALAF walipomkamata,”alisema mmoja wa wafanyabiashara.
Wafanyabiashara hao walidai baada ya tukio hilo, magari ya polisi yalifika eneo hilo na kukamata watu ovyo wakidai kuwa wanajihusisha na uvutaji wa bangi.
“Sisi tunauza biashara ya mamilioni hapa, kuna mtu ambaye atatoa fedha zake wakati akisikia harufu ya bangi?”alihoji mmoja wa wafanyabiashara hao.
Jumla ya wafanyabiashara 21 wa sehemu ya biashara ya mbao, madirisha, milango na nondo inayojulikana kama Sudan Builidings Material ama Mapambano Sudan wamedaiwa kukamatwa na polisi katika operesheni iliyoongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Rwambano Masino, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema mtu huyo alipigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakijihami kutoka katika kundi la wananchi waliokuwa wakiwarushia mawe polisi hao waliokuwa wakiwakamata wahalifu.
Akizungumza kutoka Muhimbili, baba mzazi wa Ally, Issa Sarange, alisema madaktari wamelazimika kumuondoa risasi na meno manne mwanaye.
Alisema anachoweza kuongea hivi sasa ni kuwasihi polisi wanaopewa silaha kuwa makini na matumizi yake maana wanaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
“Inakuwaje polisi unafyatua risasi katika eneo kama hili la soko, tena umekuja kukamata wavuta bangi na walevi wa pombe tu,” alisema Sarange.

0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA