.jpg)
Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ametunukiwa cheti na wanafunzi wa vyuo vikuu vya mjini Moshi kutokana na mchango wake mkubwa wa kusaidia jamii mbalimbali sambamba na kutambua mchango wake kwa taifa.
Akiwashukuru wanafunzi hao, Mengi aliwataka kuzidisha mshikamano na kufuata yote yaliyofanywa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wanafunzi hao waliandaa matembezi ya kuadhimisha kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kilele kufanyika viwanja vya Ushirika mjini hapa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Paul Makonda, alisema kutokana na mchango mkubwa wa Mengi katika taifa ndio sababu iliyowafanya kama wasomi kumtunukia cheti hicho na kwamba, jamii inahitaji Watanzania wa aina hiyo.
“Sisi kama wasomi tunatambua mchango wako kwa taifa kutokana na misaada mbalimbali unayotoa kwenye jamii na taifa kwa ujumla…wewe ni mfano wa kuigwa na jamii ingekuwa na watu kama wewe ingekuwa na maendeleo ya hali ya juu,” alisema na kuongeza:
“Hatuna cha kukupa zaidi ya kukutunukia cheti hiki kama ishara ya kutambua mchango wako kwa taifa na tunakuombea kwa Mungu.”
Mbunge wa Viti Maalum, Stella Manyanya, alisema taifa linakabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo njaa, Ukimwi, vifo vya wajawazito na watoto, rushwa na elimu iliyopo kutokukidhi matakwa.
Manyanya aliwataka wanafunzi hususan wa kike kuepuka migomo inayojitokeza vyuo vikuu nchini, badala yake, kuzingatia masomo.
0 comments:
Post a Comment