.jpg)
Watu 14 ambao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa kimataifa wa kitapeli na kuwaliza wafanyabiashara maarufu, vigogo wa serikali na taasisi nyeti, wametiwa mbaroni Jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watu hao walikamatwa jana jioni katika ofisi zao zilizoko Mikocheni maeneo ya Coca- Cola, Jijini.
Akasema watu hao ambao wamekuwa wakiwauza madini feki ni wanawake wawili walio raia wa India, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Watanzania.
“Watu hawa tumekuwa tukiwatafuta kwa muda mrefu sana. Baada ya kuweka mtego tulifanikiwa kuwakamata jana,”akasema.
Akaongeza kuwa watu hao wanahojiwa katika vituo tofauti vya polisi Jijini Dar es Salaam.
Akasema katika mtego uliowafanikisha watu hao kukamatwa, watu hao (majina yao yamehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi), walimtapeli mfanyabiashara mmoja sh. milioni 74, baada ya kumuuzia madini.
Hata hivyo, Kamanda Kova akasema mfanyabiashara huyo alikuwa ameshawapatia Sh. milioni 57 kwa ahadi ya kumalizia kiasi kilichobaki.
Akasema watu hao wamekuwa wakijishughulisha na utapeli katika nchi za Afrika Mashariki na Kati ambapo wamekuwa wakidai kuuza madini mbalimbali.
“Katika utapeli wao huwa wanawatanguliza Wakongo na Mhindi ambaye ndiye anayejulikana kama bosi wa kampuni yao,”akasema.
Akawataka watu ambao wameshawahi kutapeliwa na matapeli hao kujitokeza kwa wingi katika Kituo cha Polisi cha Kati kuwatambua.
Kamanda Kova akasema katika uchunguzi wa awali watu hao wamekamatwa wakiwa na nyaraka mbalimbali zikiwemo mikataba na kompyuta ambazo zilikuwa zikitumika katika biashara hiyo.
0 comments:
Post a Comment