
Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unatarajia kukutana na uongozi wa Chama cha soka Zanzibar (ZFA), Jumamosi kujadili ujio wa Kombe la Dunia nchini pamoja na masuala mbalimbali ya kuuendeleza mchezo wa soka nchini.
Hatua hiyo ya TFF na ZFA kujadili ujio wa kombe imekuja baada ya wadhamini wakuu wa ujio wa kombe hilo kukubali kulipitisha kombe hilo visiwani Zanzibar.
Kombe hilo litakalofanya ziara kwenye nchi zote za Afrika linatarajia kutua nchini Novemba 19, ambapo litapitishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na baadaye kuwekwa kwenye uwanja wa Taifa,ili kutoa nafasi kwa mashabiki wa soka kulishuhudia moja kwa moja.
Kombe hilo linataraji kufika Zanzibar Novemba 22, ambapo mtu pekee atakayepata nafasi ya kulishika kombe hilo ni Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Akizungumza jijini jana, Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema kuwa lengo la mkutano wao huo ni kujadiliana juu ya kuutumia ujio wa kombe hilo kwa maslahi ya Tanzania hasa kwenye nyanja ya soka.
"Tutakutana Jumamosi kuongelea masuala mbalimbali lakini kubwa ni suala la ujio wa kombe la Dunia kama mnavyojua kombe hilo litafika Zanzibar hivyo tumeona huu ndio wakati muafaka wa kuzungumzia masuala muhimu ya soka,"alisema Mwakalebela.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kampuni ya Coca Cola Afrika Mashariki na Kati tawi la Tanzania, Rita Tsehai alisema kuwa taratibu zote za ziara ya kombe hilo zitawekwa wazi wiki ijayo, ambapo ni kweli kuwa kombe hilo litafika Zanzibar.
Tsehai alisema kuwa Zanzibar imeonekana kupiga hatua kubwa kwenye soka hasa baada ya kumtoa mchezaji bora Murshid Alley kuungana na wenzake saba wa mataifa ya Ethiopia, Zambia, Zimbabwe, Namibia, Kenya, Uganda na Afrika Kusini katika kushiriki kwenye kipindi cha luninga cha Reality Show kinachoeleza wasifu wachezaji kutoka mataifa hayo.
0 comments:
Post a Comment