.jpg)
Zaidi ya Watanzania 1,300,427 wameshiriki katika kampeni ya 'Simama na Chukua hatua dhidi ya umaskini nchini'.
Idadi hiyo imeelezwa kuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na ile ya mwaka jana ambapo ni watanzania 274,000 tu ndio walioshiriki.
Aidha, idadi hiyo ni miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa katika kampeni zilizofanyika kati ya Oktoba 16 hadi Oktoba 18 mwaka huu.
Hayo yameelezwa na Bw. Musa Billegeya ambaye ni Mratibu wa Kampeni wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar.
Billegeya ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kufikisha ujumbe kwa mamlaka na wadau husika ambao wako katika nafasi ya kufanya maamuzi, hususan Serikalini.
Akasema uthibitisho wa kwanza ni kuhudhuria kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo ambapo wadau na makundi mbalimbali yalimueleza hoja na mapendekezo kwa Serikali na nini kifanyike.
"Waziri pia alikiri kuelewa hoja na ujumbe wa wananchi hao na kuahidi kuwa Serikali itafanyia kazi," amesema Billegeya.
Pia kampeni hizo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikisha ujumbe kuhusiana na hali ya umaskini nchini na haja ya kupambana na hali hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Mara, Kigoma, Lindi, Tanga na Zanzibar nayo ilishiriki katika kampeni hizo.
Kitaifa kampeni hizo zilifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar.
0 comments:
Post a Comment