
RAIS bora Afrika, anatarajiwa kujulikana Oktoba 19, baada ya Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan, kumtangaza mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim.
Hafla ya kumtangaza mshindi wa mwaka huu, itafanyika jijini London, Uingereza mbele ya wajumbe wa Kamati ya tuzo hiyo inayoongozwa na Annan, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Salim Ahmed Salim.
Wajumbe wengine wa tuzo hiyo yenye heshima kubwa ulimwenguni, ni Rais wa zamani wa Finland, Martti Ahtisaari, Waziri wa zamani wa Elimu wa Guinea, Aicha Bah Diallo, Kansela wa Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Elimu Msumbiji, Graca Machel, Mahammed Elbaradei ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomiki na Rais wa zamani wa Ireland, Mary Robson.
“Hii ni mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa tuzo hii mwaka 2006, ambapo mwaka 2007 Rais wa Msumbiji, Joaquim Chissano alitwaa tuzo hiyo. Mwaka jana, tuzo hiyo ilichukuliwa na Rais wa kwanza wa Botswana, Festus Gontebanye Mogae,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mo Ibrahim Foundation.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tuzo hiyo ni kubwa ulimwenguni ambapo ilianzishwa kwa kutambulisha na kukubali kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa Kiafrika.
Aidha, inawatunuku viongozi wa Kiafrika waliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na kutawala kwa mujibu wa katiba za nchi zao na kumaliza utawala wao kwa muda usiopungua miaka mtatu.
Tuzo ya Mo Ibrahim iliyoanzishwa mwaka 2006, ina lengo la kuchochea uongozi unaozingatia dhana ya utawala bora kwa marais wa Afrika.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja marais waliopendekezwa na kamati hiyo kuwania tuzo hiyo.
Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, aliwahi kupendekezwa mara mbili, lakini alishindwa.
0 comments:
Post a Comment