TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Saturday, October 17, 2009

Mbunge ajenga kituo cha Polisi

11:14 AM

WANANCHI wa Kata ya Kilema, Wilaya ya Moshi Vijijini wamempongeza Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Cyril Chami, kwa kuwezesha ujenzi wa kituo cha kisasa cha Polisi kilichogharimu sh milioni 300.

Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea jimbo hilo jana, wananchi hao walisema kujengwa kwa kituo hicho kutasaidia kupunguza wimbi la ujambazi uliokithiri katika eneo hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Elia Saria, ambaye anasimamia ujenzi huo, alisema kituo hicho kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi ambao wamekuwa wakililia kituo hicho.

Naye Diwani wa kata hiyo, Martin Mallya, alisema ujenzi huu umekuja wakati muafaka kutokana na eneo hilo kukosa kituo cha Polisi kwa muda mrefu, licha ya wabunge waliotangulia kushindwa kujenga.

“Tumekuwa hapa kwa kipindi kirefu bila ya kituo cha Polisi, tunamshukuru Mbunge wetu, Dk. Chami kwa wazo lake la kutujengea kituo hiki, imekuwa faraja kubwa kwa wananchi wa eneo hili,” alisema Mallya.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi walipokea wazo hilo vizuri na kuanza kukusanya mawe na mchanga, jambo ambalo limefanikisha ujenzi huo.

Kituo hicho cha kisasa kimejengwa katika Kijiji cha Mkomilo, kina nyumba tatu za kisasa ambazo zinaweza kuchukua familia tatu kwa wakati mmoja.

“Nyumba zimekamilika kama mlivyoziona zinaweza kuchukua familia tatu kwa wakati mmoja, zimejengwa katika viwango vinavyotakiwa… tunaamini askari watakaoletwa hapa hawatakuwa na shida tena,” alisema Diwani Mallya.

Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Michael Makoi, alisema kitendo cha mbunge wao kujenga kituo hicho kitasaidia wimbi la vibaka ambalo limekuwa likishamiri kila kukicha.

Tulikuwa na kazi ya kutoka hapa kwenda mjini ambako ni umbali wa zaidi ya kilomita 30, sasa tunaona tumepata mkombozi, hata lile wimbi la majambazi kukamatwa na kuachiwa kwa sababu ya walalamikaji kukosa nauli kwenda mjini halitakuwapo tena,” alisema Makoi.


0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA