TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU / ADVERTISE YOUR BUSINESS HERE AT CHEAP RATES | CONTACT ME: kilinyepesi@gmail.com

 photo DTB_zps7bd2662d.jpg

 photo fl_zps09337f7a.jpg


Habari Mpya:
Thursday, October 8, 2009

2:04 PM

Muhimbili yapandisha gharama za matibabu


Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandisha gharama za matibabu na huduma nyingine kwa wagonjwa wa rufaa binafsi (Private Patients) karibu maradufu kuanzia mwezi huu.

Huduma ambazo gharama zake zimepanda ni maabara, meno, damu, picha ya mionzi, mawimbi ya sauti, picha ya kutumia sumaku.

Gharama nyingine zilizopanda ni kulazwa, kuona daktari na upasuaji.

Kwa mujibu wa nyaraka za bei mpya kutoka Muhimbili, baadhi ya gharama za upasuaji zimepanda kufikia zaidi ya Sh. milioni moja, huku nyingine zikigota kwenye laki kadhaa.

Hata hivyo, baadhi ya gharama za huduma zimeshuka na nyingine zimebakia pale pale.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe hospitalini hapo jana, umeonyesha kuwa huduma za picha za mionzi (X-Ray) kwa upande wa figo, kibofu cha mkojo na tumbo imepanda kutoka Sh. 9,000 hadi Sh 20,000 na picha ya tumbo ya kulala na kusimama ilikuwa Sh. 9,000 na sasa imepanda hadi Sh. 20,000.

Nyingine ni picha ya magoti yote mawili ambayo imepanda kutoka Sh. 9,000 hadi Sh. 18,000, picha ya kifua ubavuni kutoka Sh. 9,000 hadi Sh. 20,000 na picha ya mifupa ya mwili mzima kutoka Sh. 12,000 hadi Sh. 40,000.

Huduma ya picha ya uti wa mgongo wote na nyonga yote imepanda kutoka Sh. 18,000 hadi Sh. 51,000.

Kwa upande wa huduma ya picha ya mawimbi ya sauti (Ultrasound), picha ya tumbo kutoka Sh. 15,000 hadi Sh. 35,000, picha ya matiti kutoka Sh.15,000 hadi Sh. 30,000, picha ya picha ya ujauzito wa dharura kutoka Sh. 15,000 hadi Sh. 25,000 na picha ya mishipa ya damu kutoka Sh. 20,000 hadi Sh. 50,000.

Kwa upande wa huduma ya picha zinazopigwa kwa mionzi baada ya kumeza dawa fulani (Fruoroscopy), picha ya uchunguzi wa kovu la kidonda kwa ndani zimepanda kutoka Sh. 20,000 hadi Sh. 35,000 wakati picha ya uchunguzi wa koromeo imepanda kutoka Sh. 30,000 hadi Sh. 40,000.

Huduma kadhaa ambazo hazikupanda ni picha ya mishipa mikubwa ya damu ambapo gharama yake ni Sh. 100,000, picha ya uchunguzi wa utumbo mpana Sh. 70,000 na CT Scan picha isiyo na rangi na yenye rangi imebakia Sh. 170,000. Picha kwa kutumia sumaku yenye rangi bila dawa gharama yake imebakia Sh. 350,000.

Gharama zilizoshuka ni pamoja na picha kwa kutumia sumaku yenye rangi na dawa ambayo imeshuka kutoka Sh. 400,000 hadi Sh. 350,000,

Akizungumza jana na Nipashe jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano wa Hospitalini ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema viwango hivyo vipya vilianza kutumika tangu Oktoba Mosi, mwaka huu.

Alisema pamoja na kupanda kwa gharama hizo, lakini bado ni nafuu kulinganisha na hospitali za binafsi.

Aligaesha alisema vigezo vilivyotumika kupandisha gharama hizo ni pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji, vifaa, tiba na matumizi mengine kwa wagonjwa.

Alitaja vigezo vingine kuwa ni kuongeza kipato cha hospitali ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa hususani wale wasiojiweza na wale ambao wanapata huduma bure bila kulipa chochote kutokana na sera mbalimbali za serikali na ongezeko la bei ya umeme, maji na kuongeza kipato kwa lengo la kutoa motisha kwa wafanyakazi.

Hata hivyo, alisema bei hizo haziwahusu wagonjwa wengine hususani wagonjwa wa rufaa, dharura na wagonjwa wanaochangia huduma.

Kwa mujibu wa Aligaesha, huduma ya wagonjwa wa rufaa binafsi (private) ilianza mwaka 1998 na bei zilirekebishwa mwaka 2003. Aliongeza kuwa tangu kipindi hicho, bei zilizokuwa zinatumika zimekuwepo kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita.

0 comments:

Post a Comment

 
BONYA HAPA