JWTZ yawaamuru raia Kunduchi wahame
Takriban watu 200 wanaoshi katika nyumba 38 zilizomo ndani ya eneo la kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam, wameamriwa kuondoka eneo hilo ndani ya siku 90 vinginevyo watang'olewa kwa nguvu.
Amri hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa Kambi hiyo, Meja Makyao kupitia barua ya Oktoba 5, mwaka huu aliowaandikia wananchi hao.
Uongozi wa kambi hiyo umesambaza nakala ya barua hiyo kwa Ofisa Mtendaji wa kata ya Kunduchi na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kunduchi Mtongani.
“Umekuwa ukiishi ndani ya eneo la kambi ya Jeshi Kunduchi Mtongani, Dar es Salaam ambalo ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania,” ilieeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
“Kwa notisi hii, unatakiwa kuondoka ndani ya eneo hilo na kuliacha wazi ndani ya muda wa miezi mitatu (siku tisini) kuanzia tarehe ya barua hii.”
Jeshi hilo lilitoa tahadhari kwamba mtu yeyote ambaye hatazingatia tangazo hilo ataondolewa kwa nguvu ifikapo Januari 5, mwakani.
Hata hivyo, amri hiyo imepingwa na wananchi hao kwa madai kwamba, wamekuwa wakiishi katika eneo hilo zaidi ya miaka 15.
Wakizungumza juzi katika ofisi za Nipashe, baadhi ya wakazi hao walisema wanasikitika kuamriwa kuondoka.
Hata hivyo, walisema awali JWTZ iliwaruhusu wananchi hao eneo hilo kwa ajili ya makaburi lakini baadhi yao wameamua kujenga nyumba, jambo ambalo walisema wanadhani huenda limechangia kuondolewa kwao.
Jumla ya nyumba 38 zinatakiwa kubomolewa katika eneo hilo la JWTZ kabla ya Januari 5, mwaka 2010
0 comments:
Post a Comment