
Dada mmoja Jijini Dar amekutwa na makubwa baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kutwangwa na nondo kichwani kufuatia kile anachodai mwenyewe kuwa ni ugomvi ulioanzishwa na mpangaji mmoja wanaeishi naye kwenye nyumba yao iliyopo Ubungo Jijini.
Dada huyo aitwaye Atugalile Mbapa, 21 (pichani mbele), hivi sasa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, MOI, ambako anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na balaa hilo la kipigo.
Akizungumza na mwandishi, Atugalile amesema amekutwa na mkasa huo hivi karibuni, majira ya saa 4:00 asubuhi pale nyumbani kwao Ubungo Bakwata.
Akieleza zaidi, akasema kabla ya tukio hilo, mama yake ambaye ndiye mmiliki wa nyumba hiyo, aliamua kufunga choo kwa kufuli ili kudhibiti wingi wa watu kutoka nje ya nyumba hiyo kuingia chooni kwao kila mara na hivyo kusababisha choo chao kiwe kichafu.
Akasema baada ya kuweka kufuli hiyo na kuweka funguo kwa juu kama ilivyo kawaida, ndipo mmoja wa wapangaji wake wanaoishi ndani ya nyumba hiyo akamzukia ghafla (mama yake) na kuanza kumpakia mitusi, akilalama ni kwanini mlango wa choo umefungwa.
"Mama alifanya hivyo kwa nia njema tu... lakini huyo mpangaji akaanza kumsemea hovyo na kuchukua nondo ili kuuvunja. Nilipojaribu kuingilia, ndipo aliponivamia na kuanza kunipiga na nondo na kuniumiza," akasema.
"Nilipomuuliza kwanini anavunja komeo badala ya kufungua na ufunguo, ndipo aliponijia juu na kuniambia nisiseme chochote kwa kuwa mimi sio mama mwenye nyumba, hivyo nimuache afanye kazi yake," akaongeza kusema.
Akaeleza zaidi kuwa kipigo hicho kiliendelea hadi watu zaidi walipojitokeza kumsaidia, lakini wakati huo tayari alikuwa ameshapoteza fahamu baada ya damu nyingi kumwagika.
Kaimu Afisa Uhusiano wa MOI, Bi. Mary Ochieng, amesema mgonjwa huyo alifikishwa hapo siku akiwa taabani lakini na baada ya kufanyiwa uchunguzi, imebainika kuwa amepata majeraha makubwa kichwani.
0 comments:
Post a Comment