Wanafunzi 230 wakosa mtihani kwa utoro na mimba
Wanafunzi 230 kati ya 7,246 waliofanya mtihani kwa kumaliza darasa la saba mwaka huu wilayani Handeni, wameshindwa kufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mimba.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake jana kuhusu maendeleo na changamoto mbalimbali zinazoikabili Idara yake, Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani hapa, Ali Selemani Mwegole, alisema wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 7,010 ambapo wasichana ni 3,401.
Mwegole alisema utoro umeathiri zaidi watoto wa kike ambapo jumla yao ni 122 na wavulana 81. Waliopata ujauzito na kusababisha waache shule ni 15 huku vifo vikihusisha watoto wawili, wakike na wakiume.
Alisema kuwa watoto tisa wakiume watano na wasichana wanne waliugua na kushindwa kufanya mtihani huo huku mvulana mmoja pekee kufukuzwa shule kutokana na utovu wa nidhamu.
"Tunatarajia kwamba jumla ya wanafunzi 5,796 watafaulu na kujiunga na kidato cha kwanza mwakani. Mahitaji yetu ni jumla ya vyumba 145 vya madarasa ya kidato hicho, alisema Mwegole.
Naye Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari wilayani hapa Simon Mdaki, alisema wana upungufu wa vyumba 44 vya madarasa, vyumba vilivyopo ni 109.
0 comments:
Post a Comment