.jpg)
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi lililotolewa na vigogo wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 104.1, kwamba hawastahili kushtakiwa kutokana na kifungu cha sheria namba 65 kinachowapa kinga mtumishi kushitakiwa kwa makosa aliyotenda akitekeleza majukumu ya kazi.
Mahakama hiyo imesema washtakiwa walitenda makosa yanayowakabili wakiwa na nia ovu ya kumpotosha mwajiri wao na sio kwa nia njema kama kifungu hicho cha sheria kinavyosema.
Washtakiwa hao ni wakurugenzi wa vitengo kadhaa vya BoT ambao ni Simon Jengo, Kisima Kimango, Bosco Kimela na Ally Bakari.
Uamuzi huo ulisomwa jana na Hakimu Mkazi Samuel Maweda wa mahakama hiyo.
Hakimu Maweda alisema wakili wa utetezi anaelewa kwamba kesi hiyo imefikishwa mahakamani hapo chini ya kifungu namba 29 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa ajili ya usikilizwaji wa awali ambapo upelelezi utakapokamilika itahamishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alisema ni sahihi kupokea hoja wakati kesi hiyo iko katika hatua ya usikilizwaji wa awali, lakini wakili wa washitakiwa, Mpare Mpoki, alikosea kutoa hoja zake kabla washtakiwa hawajasomewa mashitaka yanayowakabili.
"Kwanini wakili wa utetezi atoe hoja kabla washitakiwa hawajasomewa mashitaka, wakati washitakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nia ovu hivyo kifungu hicho hakiwezi kuwakinga. Mahakama hii inatupilia mbali pingamizi lao," alisema Hakimu Maweda.
Hata hivyo, wakili Mpoki alisema anakata rufaa kupinga uamuzi huo ambapo aliomba nakala ya uamuzi.
Awali, washitakiwa hao walisomewa mashitaka yao na Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Beni Rinkolini, ambaye alidai kuwa mshitakiwa wa kwanza Jengo akiwa Mkurugenzi wa BoT na wa pili, Kimango akiwa Naibu Mkurugenzi wa fedha, mwaka 2004 kwa lengo la kumdanganya mwajiri, waliandaa rasimu ya ziada kwa wasambazaji wa noti yenye mkataba wa mwaka 2001, kwa lengo la kumpotosha mwajiri wao.
Rinkolini alidai kuwa, mwaka 2005 mshitakiwa wa kwanza akiwa mtumishi wa umma aliagiza kuchapishwa kwa thamani kubwa ya fedha ikilinganishwa na iliyoandaliwa na kitengo cha BoT akiwa na lengo la kumpotosha mwajiri wake.
Katika shitaka la tatu, washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kwa kutumia nyadhifa zao, walishindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuandaa rasimu ya ziada yenye mkataba wa mwaka 2001 ilionyesha thamani ya juu wa kuchapisha kiwango cha noti kuliko mkataba halali unavyoeleza.
Ilidaiwa kuwa kwa kitendo cha washitakiwa kufanya hivyo, kiliisababishia serikali hasara ya Sh. 104,158,536,146.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Katika hatua nyingine, askari magereza jana waligeuka kuwa mabaunsa kwa kulinda mlango wa mahakama na kuwasukuma waandishi wa habari wasiingie mahakamani kuripoti mwenendo wa kesi hiyo.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kuwaingiza washitakiwa hao katika chumba cha mahakama ambapo zaidi ya askari 10 waliingia na wengine kuzuia mlangoni huku wakiwasukuma wanahabari kutoka vyombo mbalimbali.
Hata hivyo, waandishi wa habari walilazimika kuzunguka nyuma ya jengo hilo ili kusikiliza kesi hiyo kupitia dirishani, lakini askari wengine walijitokeza na kuzuia wanahabari kutekeleza wajibu wao wa kuripoti mwenendo wa kesi hiyo kwa lengo la kuwapasha habari wananchi.
Kutokana na kitendo hicho, Hakimu Maweda alilazimika kuingilia kati na kuamuru askari hao kuwaacha waandishi wa habari kusikiliza kesi hiyo kupitia dirishani.
Kesi hiyo imeahirishwa na itatajwa Oktoba 2, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment