
Mbunge wa jimbo la Geita, Bwana Ernest Gakeya Mabina amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na kuombwa kuacha kutumia mikutano ya Serkali kujinadi kwenye mkutano wa hadhara.
Sakata hilo lilitokea majuzi kwenye uwanja wa Kalangalala wakati mheshimiwa huyo alipokuwa anajibu maswali ya wananchi.
Kimbembe cha kumzomea mheshimiwa huyo, kilitokea baada ya wananchi kumlima maswali kadhaa na kupokea majibu ambayo hawakuridhika nayo.
Licha ya kumzomea, baadhi walianza kuondoka kwenye uwanja huo wa mkutano huku wakipiga miruzi.
Baadhi ya maswali aliyoulizwa na wanachi kwenye mkutano huo wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi kiduchu ni pamoja na kutaka kufahamu mbunge huyo amezaliwa wapi na makazi yake yako wapi?
Kadhalika walitaka kufahamu watoto wa mheshimiwa huyo wanasomea wapi kutokana na kile kilichodaiwa kuwa hana uchungu na jimbo lake kutokuwa na makazi yake kuwa Jijini Dar es Salaam.
Uzomeaji ulianza tu pale alipowaambia wananchi wakati akijibu swali la mwananchi aliyetaka kufahamu wabunge wa Geita inakuwaje wanapochaguliwa wanakwenda kimoja mpaka uchaguzi mkuu unapaokaribia ndipo wanaonakena tena majimboni.
Mwananchi mwingine alimtaka mbunge huyo kuacha tabia ya kutumia mikutano ya Serikali kama huo ulivyokuwa umetambulishwa kujinadi yeye na CCM badala ya kuzungumzia Serikali imewafanyia nini wananchi.
Mwananchi mwingine alimhoji mbunge huyo kama kwenye huo mkutano alikuwa amekuja kujinadi au kusikiliza kero za wananchi na kudai kuwa amekuwa anawataka wananchi wakiwemo walimu wampe kura wakati hafahamu matatizo yao.
Hata hivyo kabla ya kujibiwa kwa maswali hayo yote, kelele za kuzomea zilitawala mkutano huo na kumfanya Mbunge huyo kukatisha katisha hotuba yake.
Wakati wananchi wakitoka uwanjani huku wakizomea na kupiga miruzi, Mbunge huyo alionyesha ujasiri kwa kuendelea kuhutubia tena wananchi wachache waliokuwa wamebakia uwanjani hapo.
0 comments:
Post a Comment