Kigogo shirika la ndege mbaroni kwa kuua mtu
Meneja wa Shirika la Ndege la Ethiopia Airline, Bw. Mecked Libeche, 40, mkazi wa Mikocheni, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kusababisha ajali iliyoua mtu mmoja papo hapo Jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile amesema Mkurugenzi huyo anadaiwa kusababisha ajali hiyo mishale ya saa 1:00 usiku, katika eneo la FK Motors, Vingunguti, kwenye barabara ya Nyerere Jijini.
Akamtaja mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Salum Ally, 40, mkazi wa Jet Club.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Shilogile amesema mida hiyo Mkurugenzi huyo alikuwa akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere akielekea mjini akiendesha gari lenye namba za usajili T 970 ANB aina ya Rav4.
Akasema alipofika eneo la FK Motors pale Vingunguti, akamgonga Salum ambaye alikuwa akiendesha baiskeli akitokea Uwanja wa Ndege kwenda Jeti.
Kamanda Shilogile amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Chumba cha Kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Amana.
Akasema hivi sasa, Mkurugenzi huyo anashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi na kuwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment