
Kesi ya mauaji ya albino na vikongwe zilizoahirishwa kusikilizwa mapema Julai, mwaka huu, katika Mahakama Kuu maalum za Kahama na Shinyanga, zinaanza kusikilizwa tena leo.
Katika Mahakama Kuu maalum ya mjini Shinyanga, usikilizaji wa kesi hiyo ulisitishwa baada ya Jaji Gadi Mjemas kufiwa na mama yake mzazi na kwamba kuendelea kusikilizwa kulisubiri taarifa ya Msajili wa Mahakama.
Hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alinukuliwa na vyombo vya habari akisema serikali imetenga bajeti ya kutosha ya kuendesha kesi hizo na kilichosababisha zisimame, lilikuwa ni tatizo la Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kufiwa na mama yake mzazi.
Kesi hiyo ya mauaji albino Lyaku Willy inawakabili washtakiwa wanne ambao ni Mboje Mawe, Chenyenye Mangayale, Sayi Gamanya na Sayi Mofizi.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali, Edwin Kakolaki, aliieleza Nipashe kuwa leo shahidi wa pili katika kesi katika kesi hiyo ambaye anadaiwa kuwa alikuwa mkuu wa upelelezi wilaya ya Bariadi, Foca Dinyo anatoa ushahidi wake.
Wakati kesi hiyo ikiahirishwa Julai 13, tayari shahidi wa 12 D 7316 Koplo Ernest wa upande wa mashitaka alitoa ushahidi wake lakini upande wa utetezi ulipinga maelezo ya shahidi kutolewa kama kielelezo namba 10.
Baada ya upande wa utetezi kupinga kutolewa kwa maelezo hayo ulipelekea kuanza kusikilizwa kwa kesi ndani ya kesi.
Katika Mahakama Kuu maaluum ya mjini Kahama, kesi za mauaji ya albino na vikongwe zinasikilizwa na Jaji Gabriel Rwakibalila baada ya Msajili wa Mahakam Kuu kuzipangia tena muda wa kuendelea kusikiliza kesi namba 24, 25 na 26 za mauaji ya kukusudia ya albino na vikongwe katika Mahakama za Kahama na Shinyanga.
Kuendelea kwa kesi hizo katika mahakama kuu mjini hapa, kunautaka upande wa utetezi kuhakikisha kuwa mashahidi wao wanafika mahakamani leo kama ilivyosisitizwa na Jaji Rwakibalila wakati akiahirisha kesi hizo Julai 13 mwaka huu.
Kesi hizo ni namba 24/2009 ya mauaji ya kijana Matatizo Dunia inayo wakabili Masumbuko Madata wa Ituga, Emmanuel Masangwa wa Bunyihuna na Charles Kalamuji au Masangwa wa kijiji cha Nanda wote wa wilayani Bukombe kwa kuhusika na mauaji hayo ya kukusudia ya Desemba mosi, 2008 katika kijiji cha Bunyihuna.
Kesi nyingine ni namba 25 ya mauaji ya mtoto Esther Charles (13) wa kijiji cha Shilela kata ya Segese tarafa ya Msalala yaliyotokea Oktoba 2008, inayowakabili washitakiwa watano wakiwemo pia Masumbuko Madata na Charles Kalamuji na Merdad Maziku Machunda wa mjini Kahama, Malalija Jitunga. al maarufu ‘Katare' na Peter Malima al maarufu “Mugabe” wote kutoka wilayani Kahama.
Kesi nyingine ni nambari 26 ya mauaji ya kikongwe Ng’wana Gimbishi (75) mauaji ambayo yanadaiwa yalitokana na imani za ushirikina inayomkabili mkazi mmoja wa kijiji cha Kagongwa kata ya Isagehe wilayani Kahama, Joseph Lugata yaliyotokea Januari 8, 2009 katika kijiji cha Kilimbu kata ya Mwalugulu wilayani hapa ambapo inadaiwa Lugata alimuua kwa kukusudia bibi huyo.
Leo upande wa utetezi katika kesi namba 24 inayowakabili Madata na wenzake unatarajiwa kuwaleta mashahidi wake watano na kutoa ushahidi wao dhidi ya mshitakiwa Masumbuko Madata, Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji na kesi ya mauji ya Shilela nayo kuanza kusikilizwa.
Habari hii imeandikwa na Grace Chilongola, Shinyanga na Ancet Nyahore, Kahama.
0 comments:
Post a Comment