.jpg)
Kuna habari kuwa vigogo kadhaa waliokuwa wachapa kazi wa kutumainiwa katika Ikulu ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa watatinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kutoa maelezo ya kina kuhusiana na kesi ya aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzie.
Hivi sasa, Mramba anakabiliwa na kesi inayohusiana na kutumia madaraka vibaya na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni 11.7, sambamba na Waziri mwingine wa zamani katika Wizara ya Fedha, Daniel Yona na pia aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gray Mgonja.
Chanzo cha Alasiri kinadai kuwa vijana zaidi wa Mkapa watatinga kortini baada ya washtakiwa Mramba, Yona na Mgonja kutaja mashahidi wao wa utetezi.
"Mramba aliwahi kusema kortini kuwa maamuzi yake kuhusiana na msamaha wa kodi kwa kampuni ya Alex Stewart yana baraka za Ikulu (ya Rais Mstaafu Mkapa)... sasa ushahidi utakapotakiwa, ni wazi kwamba kuna vigogo waliokuwa ikulu wakati huo watatakiwa kutinga kortini ili kutoa ushahidi wao," kimedai chanzo hicho.
Jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, upande wa Serikali ulishaanika majina ya mashahidi wake 17 ambapo miongoni mwao, ni pamoja na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mramba katika wizara hiyo ya fedha, Abdisalaam Issa Khatib.
Khatib na mashahidi wengine 16 wanatarajiwa na upande wa Serikali kutoa ushahidi juu ya tuhuma za Mramba na wenzie (Yona na Mgonja).
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Herbert Nyange, ulipinga kutaja mashahidi wake na kudai kuwa kwa kufanya hivyo, itakuwa ni kinyume cha sheria, kwa mujibu wa mwongozo uliowahi kutolewa na aliyekuwa Jaji Mkuu mwaka 1992, Marehemu Francis Nyalali.
Baada ya madai hayo ya upande wa utetezi, jopo la mahakimu wanaosikiliza shauri hilo, wakiongozwa na Hakimu Mkazi John Utamwa waliamua kutoa muda kwa upande wa Serikali kusoma mwongozo huo kwa makini na kuwataka leo wafike mahakamani wakiwa na hoja za msingi za kujibu pingamizi hilo.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, kesi hiyo ilikuwa haijaanza kurindima katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ingawa akina Mramba walikuwa wameshafika mahakamani hapo.
Akina Mramba wanakabiliwa na kesi inayohusiana na kutumia madaraka yao vibaya na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya Alex Stewart, kinyume na taratibu na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 11.7.
0 comments:
Post a Comment