Waandishi wanaoandika habari za uchochezi waonywa
Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kutumia uhuru wa habari uliopo kuandika habari zenye maslahi kwa taifa na ambazo hazichochei chuki, uhasama na kutishia uvunjifu wa amani.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Clement Mshana, wakati wa sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo cha Uandishi wa Habari cha Times, cha Jijini Dar es Salaam.
Amesema vyombo vya habari nchini vinao uhuru mkubwa wa kutangaza habari zozote ili mradi havivunji sheria za nchi kwa kuandika habari ambazo kwa namna moja au nyingine hazizingatii taaluma ya uandishi wa habari.
“Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitumia uhuru uliopo na kuandika habari ambazo hazina maslahi kwa taifa letu, habari hizi ni pamoja na zinazochochea chuki, uhasama na kutishia uvunjifu wa amani,’’ akasema Bw. Mshana.
Amefafanua kuwa Tanzania kwa muda mrefu imekuwa kisiwa cha amani tangu ipate uhuru wake mwaka 1961 na kwamba amani iliyopo haikuja tu kwa bahati, bali imetokana na juhudi za waasisi wa taifa hili wakionngozwa na Baba wa Taifa, Mwl Julius Kambarage Nyerere aliyepiga vita ukabila, udini, ubaguzi wa rangi na pia kukemea tabia ya baadhi ya watu wachache kujilimbikizia mali.
Amesema Tanzania bila amani hakuna maendeleo na juhudi zote zinazofanywa na viongozi zikiwemo za kilimo kwanza, MKUKUTA na nyinginezo, haziwezi kutekelezwa endapo amani ya itatoweka.
“Juhudi zote zinazofanywa hivi sasa za viongozi wa kuhimiza kilimo kwanza, MKUKUTA na nyinginezo, haziwezi kutekelezwa endapo amani itatoweka, kwa bahati nzuri watu wa kulinda amani isitoweke ni ninyi wana habari” akasema.
Kadhalika Bw. Mshana aliwataka wana habari kote nchini kuwa makini na kujiepusha na habari zinazochochea uhasama ndani ya jamii ili kuhakikisha kuwa jamii ya Watanzania inaendelea kuishi katika hali ya amani na utulivu.
0 comments:
Post a Comment