.jpg)
Hofu imetanda kwamba wanafunzi kadhaa wa Shule ya Kimataifa Tanganyika jijini Dar es Salaam, wanaugua ugonjwa wa mafua ya nguruwe.
Kufuatia hofu hiyo, jana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ililazimika kutuma timu ya wataalam wake katika shule hiyo kwenda uchunguza madai hayo.
Ofisa Habari Mwandamizi wa wizara hiyo, Nsachris Mwameja, alisema timu hiyo ya wataalam tayari inafanya uchunguzi shuleni hapo na taarifa kuhusu suala hilo itatolewa baadaye.
Habari za awali ambazo Nipashe ilizipata zilidai kwamba wanafunzi takriban saba wa shule hiyo wanaugua ugonjwa huo.
Ilidaiwa kwamba baada ya kubainika kuwa wanaumwa ugonjwa huo, wanafunzi hao walikimbizwa na kwenda hadi katika kliniki ya IST iliyopo Mtaa wa Chole, eneo la Masaki, wilayani Kinondoni kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wanafunzi hao ni raia wa kutoka nje ya Tanzania na kwamba walibainika kuugua ugonjwa huo baada ya kuwasili nchini wakitoka kwao ambako walikwenda kwa likizo.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa shule hiyo, David Showver, alisema madai hayo hayana ukweli wowote na mwenye mamlaka ya kutoa habari hizo ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Alisema hakuna mwanafunzi aliyelazwa katika kliniki yao akiugua ugonjwa huo.
Taarifa zaidi zilidai kuwa, wanafunzi hao wameendelea kupatiwa matibabu katika kiliniki hiyo kwa zaidi ya siku nne na kwamba mfanyakazi mmoja wa shule hiyo ambaye ni Mtanzania, ameambukizwa na kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Lakini kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma ya Tiba (MNH), Profesa Andrew Swai, hakuna mgonjwa wa mafua ya nguruwe anayepokelewa hospitalini hapo.
Baada ya kuwapo kwa tetesi za wagonjwa hao, wafanyakazi wa shule hiyo, wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kutoa taarifa mapema endapo watakuwa na dalili za ugonjwa huo.
Aidha, imedaiwa kuwa wafanyakazi hao wamepewa vipeperushi vinayoelezea kuhusiana na dalili za mafua ya nguruwe, jinsi ugonjwa huo unavyoambukiza na namna ya kujikinga.
0 comments:
Post a Comment